1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wananchi wa Ugiriki kuandamana

Kabogo Grace Patricia5 Machi 2010

Maandamano hayo yatawahusisha wafanyakazi wa idara za serikali, ofisi za manispaa, hospitali, mabenki na shule.

https://p.dw.com/p/MKjP
Waziri Mkuu wa Ugiriki, George Papandreou.Picha: AP

Wananchi wa Ugiriki leo wanafanya maandamano ya kupinga mpango uliopendekezwa na serikali ya nchi hiyo katika jitihada za kupunguza gharama zake. Imeelezwa kuwa idara mbalimbali za serikali, ofisi za manispaa, hospitali, mabenki na shule zitafungwa, huku huduma za usafiri zikiathiriwa pia.

Mgomo huo utakaodumu kwa muda wa saa tatu uliotishwa na vyama vya wafanyakazi wa mashirika ya umma na yale binafsi, utaishinikiza kufungwa kwa wizara za serikali, ofisi za manispaa na mabenki kuanzia muda wa mchana, huku shule zikifungwa kwa siku nzima ya leo. Wiki hii serikali ya Ugiriki ilitangaza kupunguza gharama zake kwa hadi euro bilioni 4.8, kufuatia shinikizo la Umoja wa Ulaya na masoko ya fedha ya kimataifa, ili kurejesha imani kwao. Hatua hiyo ya serikali ya Ugiriki ni katika kujifunga mkaja ili kuinusuru nchi hiyo kufilisika kutokana na deni lake.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Ujerumani la DPA, hospitali nchini Ugiriki zimebakiwa na madaktari kwa ajili ya dharura kufuatia madaktari wengine kushiriki katika maandamano hayo. Imeelezwa kuwa waandishi habari nao watakuwa miongoni mwa waandamanaji. Huduma za treni na mabasi zimefutwa nchi nzima kwa muda wa saa 24. Mashirika ya ndege ya Olympic na Aegean yamesema yamelazimika kufuta zaidi ya safari 20 za ndege na kuabdilisha muda wa safari nyingine 74 ndani ya nchi hiyo na zile za nje ya nchi. Vyama vikubwa viwili vya wafanyakazi nchini Ugiriki vinavyowakilisha takriban wafanyakazi milioni 2.5, au karibu nusu ya nguvu kazi ya taifa, wametoa mwito kwa wafanyakazi hao kuandamana hii leo na pia kugoma kwa muda wa saa 24 tarehe 16 ya mwezi huu wa Machi.

Papandreou kuzuru Ujerumani

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Ugiriki, George Papandreou hii leo anatarajiwa kufanya ziara nchini Ujerumani kwa mazungumzo na Kansela Angela Merkel, kiongozi wa nchi iliyo na uchumi mkubwa kabisa barani Ulaya kwa lengo la kutafuta kuungwa mkono kisiasa kutokana na mkakati wake mpya wa kiuchumi. Akizungumzia hatua hiyo, Papandreou alisema, ''Lazima turejeshe ile imani iliyopotea juu ya nchi yetu. Katika miezi inayokuja tuna wajibu wa kufanya kazi kwa pamoja ili kudhihirisha kwamba sisi hatutegemei watu wengine na kwamba sisi kama wananchi na nchi tunaweza kuamua juu ya mustakabali wetu.''

Mpango huo mpya wa Ugiriki wa kupunguza matumizi ya bajeti yake utahusisha kupunguza gharama za sekta ya umma kwa asilimia 30, kusitisha malipo ya uzeeni na kuongeza kodi kwa bidhaa zisizo muhimu kama vile pombe na sigara.

Ugiriki sasa inasubiri kuungwa mkono na Umoja wa Ulaya baada ya kutangaza mpango wake huo. Deni la euro bilioni 300 la Ugiriki limeitikisa sarafu ya euro, huku nchi washirika wake wa Umoja wa Ulaya zikihofia kwamba soko ambalo si thabiti linaweza kusambaa katika nchi zinazotumia sarafu ya euro ambazo zina madeni makubwa kama vile Uhispania na Ureno.

Mwandishi: Grace Patricia kabogo (DPAE)

Mhariri: Othman Miraji