1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanasayansi watathimini athari za kuyayuka barafu katika maeneo ya barafu duniani

Mohammed Abdul-Rahman2 Machi 2007

Tangu Alhamisi wiki hii wanakusanyika wanasayansi mjini Berlin kutathimini hali ya mazingira duniani katika kile kinachojulikana kama mwaka wa kimataifa wa eneo la barafu la sayari ya dunia. Ni juhudi kubwa kabisa ya utafiti kuwahi kuonekana katika kipindi cha miaka 50 kuhusu pembe za barafu duniani.

https://p.dw.com/p/CHlY
Meli ikiasafiri katika mojawapo ya maeneo ya barafu duniani inayozidi kuyayuka.
Meli ikiasafiri katika mojawapo ya maeneo ya barafu duniani inayozidi kuyayuka.Picha: DW-TV

Harakati hizo kwa hakika zitaendelea hadi 2009 na zinaratibiwa kote duniani , katika wakati ambao Ulimwengu unazidi kushuhudia kuharibiwa mazingira na kuongezeka kwa hali ya ujoto.

Mwenyekiti wa kamati ya ujerumani ya kila kinachojulikana kama mwaka wa kimataifa wa maeneo ya barafu duniani- International Polar Year, Reinhard Dietrich anasema upande wa kiza wa mwezi unafahamika vyema zaidi kuliko nyanja nyengine za maeneo ya barafu. Anaona kuna haja kubwa ya kufanya utafiti mpana zaidi ili kupata maarifa juu ya pembe za barafu za dunia, hasa panapohusika na athari za kuyayuka barafu kwa mazingira.

Katika hatua hiyo ambayo ni ya aina yake wanasayansi wapatao 50,000 kutoka sehemu zote duniani watashiriki katika miradi 200 tafauti katika maeneo ya barafu ulimwenguni, kwa utafiti unaoanzia katika sehemu za mapande ya barafu huko Greenland, hadi katika kupima mawimbi ya kasi ya bahari, pamoja na mipango ya kuwalinda bweha katika maeneo ya barafu pamoja na ndege aina ya pengwini wanaoishi katika maeneo hayo.

Alfred Sachs kutoka taasisi ya Alfred Wegener inayohusika na utafiti wa maeneo ya barafu na bahari kwa mfano, ataendelea kuchunguza juu ya kuwepo kwa gesi aina ya methane katika kanda za dunia na hatari ya kuzitoa gesi hizo katika kipindi cha kuyayuka kwa maeneo ya barafu.Allfred Sachs anasema :-

"Nina angalia utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira kutoka maeneo hayo . Hii ni muhimu kwa sababu organic carbon hurundikana katika maeneo hayo. Wakati maeneo hayo aya barafu yabaelekea kuyayuka zaidi na zaidi, gesi ya carbon inakua rahisi kutoka. Lakini bado haieleweki wazi chanzo hicho kina nguvu kiasi gani na kinaweza kuwa na athari gani .“

utafiti wa kisayansi utakaofanywa wakati wa muda wote wa mradi huu wa kimataifa, utatumika pia kuweza kupata maarifa zaidi kuhusu kiwango cha mabadiliko ya hali ya hewa kilivyo kwa wakati huu. Kuna watu wengi pia wanaoamini kwamba mchango wa binaadamu katika mabadiliko ya mazingira si jambo linalopingika,kwa maneno mengine binaadamu anachangaa katika uchafuzi wa mazingira.

Kwa upande mwengine wa tukio hili linalofanyika Ujerumani la kuanza kwa maadhimisho ya mwaka wa kimataifa ya maeneo ya barafu,ni dai la kundi la waakilishi kutoka maeneo hayo, wakiwa ni waakazi asilia wa maeneo hayo kutaka wawe na usemi zaidi katika miradi ya utafiti katika maeneo yao, wakisisitiza kwamba wao ndiyo wa kwanza wanaoonja machungu ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa na mazingira kwa jumla.Gerth Peoten kutoka Greeland ni miongoni mwao , anasema kuwa :-

"Niko hapa leo kuwaonyesha wanasayansi na jumuiya, kwamba watu wa eneo la barafu wanapaswa kusikilizwa. Kunapaswa kuwepo na ushirikiano wa karibu zaidi miongoni mwa watu asilia wa maeneo hayo na wanasayansi. Tunachotaka tu ni kuonyesha kwamba na sisi pia tupo hapa na kuwa tunataka pia kuleta mabadiliko .“

Juhudi zote hizi zinatokana na muamko unaozidi juu ya kitisho cha ongezeko la joto duniani na kuzidi kuharibiwa mazingira kwa jumla pamoja na haja ya kuchukuliwa hatua za dharura kuinusuri sayari hii-dunia.