1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanasiasa wa Ujerumani wanapata mishahara kiasi gani?

Zainab Aziz
23 Septemba 2017

Wanasiasa hawalali njaa nchini Ujerumani hilo ni wazi kabisa. Je nani anapata kiasi gani na kansela Angela Merkel anapokea kiasi gani kulinganisha na viongozi wengine wa serikali?

https://p.dw.com/p/2kZYT
Deutschland Wahlkampf CSU/CDU auf dem Marienplatz in München
Picha: picture alliance/dpa/S. Hoppe

Mfumo wa malipo kwa wanasiasa nchini Ujerumani, hauko wazi kabisa. Kwa kawaida wabunge hawalipwi mishahara kwa kazi zao lakini hulipwa posho ili kukimu gharama zao. Wabunge wanapokea euro 9542 kila mwezi na juu yake wanapokea euro 4318 ambazo hazikatwi kodi, fedha hizo ni kwa ajili ya kufidia gharama zinazotokana na mazingira yaliyomo ndani ya mamlaka ya kisiasa, kwa mfano malazi karibu na bunge "Bundestag”, chakula au gharama za usafiri.

Lakini si hayo tu: Kwa kiwango cha jumla ya euro 12,000 kwa mwaka, wabunge wanaweza kuzitumia fedha hizo kuboresha ofisi zao pamoja na kununua vifaa vitakavyohitajika kuboresha utendaji kazi wao, kama vile simu mpya za mkononi "smartphones" au mashine za kutengenezea kahawa. Hata hivyo, wabunge hupokea fedha hizo kwa masharti kwamba watathibitisha matumizi yake. 

Posho za wabunge

Posho za wabunge ziliongezwa mwezi Julai mwaka huu na sasa watakuwa wanapokea ongezeko la mshahara kila mwaka, sheria ambayo ilipitishwa tangu mwaka 2016 inayozingatia maendeleo ya jumla kuhusiana na malipo ya mishahara hapa nchini Ujerumani.

Je malipo ya mishahara yanatafautiana kivipi kwa wabunge wa mabunge ya mikoa katika nchi nzima? Je wao pia hupokea posho za kufidia gharama ambazo viwango vyake vinaweza kutofautiana kabisa?  Kwa mfano, wawakilishi wa bunge la jimbo la Hamburg hupata posho ya euro 2641 tu pamoja na fedha zingine kiasi cha euro 350.  Lakini kwa upande mwingine, wanachama wa bunge la serikali katika jimbo la "Northrhein Westphalia” wanastahiki kupata euro 9,500 kwa mwezi bila kupata marupurupu mengine ya kufidia gharama zao.

Kwa watu maalumu au kwa jina jingine "samaki wakubwa" katika biashara ya siasa hapa nchini Ujerumani kama vile  Angela Merkel, Sigmar Gabriel, Frank-Walter Steinmeier na wenzao je wao wanapaokea kiasi gani?

Bi Merkel anapokea euro 17,732  kila mwezi pamoja na posho ya euro1000 inayokidhi mahala alipo pamoja na posho nyingine za ziada. Rais wa Shirikisho Frank-Walter Steinmeier, ingawa ana kazi zaidi katika majukumu yake ya uwakilishi kwa mujibu wa tovuti ya Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani daima yeye hupata sehemu kumi na tisa ya mshahara wa Kansela wa Ujerumani. Rais Steinmeier anapokea  euro 19,719  kwa mwezi ikiwa ni pamoja na majumuisho ya ruzuku anazopokea. Mawaziri wa Ujerumani stahili yao ni euro 15,000 kwa mwezi pamoja na ruzuku wanazopewa.

Mishara ya wanasiasa wa juu

Mishahara ya wanasiasa wote wa juu inazingatia misingi ya mishahara ya kawaida na maongezeko mengine mbalimbali. Kwa mujibu wa ibara ya  § 11 ya Sheria ya Wizara za Shirikisho, kiasi hicho kinaegemea mshahara wa watumishi wa umma. Aidha, Baraza la Mawaziri la Shirikisho la Ujerumani pia linazingatia gharama ambazo hutunukiwa manaibu wa bunge la Ujerumani.  Kiasi cha euro 12,270.96 kwa mwaka kwa Kansela na euro 3,681.36 kwa mawaziri wa Shirikisho.

Kansela wa Ujerumani anapokea mshara mdogo ukilinganisha na mshahara wa rais wa Marekani kwa mwaka ambao ni sawa na euro 333,000. Waziri Mkuu wa Singapore, Lee Hsien Loong, ambaye anapata karibu euro milioni 1.5 kwa mwaka, bila shaka anapokea kiasi kikubwa kuliko anachopata kansela wa Ujerumani.

Wajerumani hata hivyo hawawezi kulinganisha mishahara ya wanasiasa wao na wale wa nchi nyingine na hasa katika mpangilio wa mishahara ya kawaida. Mishahara ya wajumbe wa baraza la Mawaziri, pamoja na ya wabunge wa kawaida, ni ya juu kuliko kipato cha wastani cha nchini Ujerumani suala ambalo linawafanya wanasiasa kulaumiwa na umma.

Kulingana na utafiti wa taasisi ya Otto Brenner kwa ushirikiano na mpango wa uwazi wa abordnetenwatch.de, kila mmoja kati ya wabunge wanne wa bunge la Ujerumani anapokea  zaidi ya euro 10,000  kwa mwaka kama posho katika kazi yake hii ya pembeni inayomlipa vizuri sana.

Mwandishi: Zainab Aziz/ Ines Eisele/ LINK: http://www.dw.com/a-40602240

Mhariri:Josephat Charo