1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaume wawili watiwa mbaroni kwa tishio la ugaidi Essen

12 Machi 2017

Wanaume wawili wamekamatwa kwa tishio la ugaidi katika mji wa magharibi wa Essen nchini Ujerumani polisi imekifunga kituo cha maduka baada ya kudokezwa na duru za usalama juu ya kuwepo kwa mpango wa kukishambilia.

https://p.dw.com/p/2Z4Mw
Polizei schließt nach Terrordrohung Einkaufszentrum
Picha: picture alliance/dpa/B. Thissen

Wanaume wawili wamekamatwa kuhusiana na tishio la ugaidi katika mji wa magharibi wa Essen nchini Ujerumani polisi imekifunga kituo cha maduka baada ya kudokezwa na duru za usalama juu ya kuwepo kwa mpango wa kukishambilia.

Polisi chungu nzima wamekizingira kituo hicho cha Limbeker Platz kilioko Essen hapo Jumamosi baada ya kutaarifiwa juu ya kile walichosema ushahidi wa kuaminika wa shambulio la kigaidi siku moja kabla.Mashirika ya usalama yaliyotajwa na gazeti la Ujerumani la Bild yamelielezea tishio hilo kuwa linaweza kuwa kujiripuwa kwa kujitowa muhanga katika vituo vingi.

Halikadhalika katika duka,eneo la kuegesha magari la karibu na hapo na kituo cha reli cha chini ya ardhi vyote hivyo vilifungwa wakati mbwa wanoafanya upekuzi kwa kutumia harufu wakilipekuwa eneo hilo.

Msemaji wa polisi ya Essen ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba "tumepokea ishara nzito kutoka kwa duru za usalama kwamba kunapangwa shambulio leo na litatekelezwa." na "ndio maana tumelazimika kuchukuwa hatua hizo."

Mkono wa Dola la Kiislam?

Einkaufszentrum Limbecker Platz in Essen
Kituo cha maduka cha Limbecker Platz mjini Essen.Picha: picture-alliance/dpa/B. Thissen

Polisi baadae iliamuru kituo hicho cha maduka ambacho ni mojawapo ya vituo vikubwa kabisa nchini Ujerumani kiendele kufungwa kwa siku nzima ya Jumamosi na kuongeza kwamba sasa wanaamini wamezima shambulio hilo.

Hapo Jumamosi polisi ilitangaza kwamba uchunguzi ulikuwa ukiendelea na kuwashukuru watu ambao waliitikia wito wao kupitia mtandao wa kijamii au kwa simu wakati wa operesheni hiyo ya polisi.

Shirika la habari la Ujerumani dpa na gazeti la "Bild" vimekariri duru za usalama zikisema njama hiyo inaaminika kuwa ni kazi ya kundi la wanamgambo linalojiita Dola la Kiislamu (IS).Duru hizo zimesema mwanaume wa Ujerumani aliyesafiri kwenda Syria kupigana bega kwa bega na kundi hilo anatuhumiwa ndiye mpangaji wa shambulio hilo lililokuwa lifanyike.Imeripotiwa kuwa alikuwa na mawasiliano na watu kadhaa katika eneo la Essen na pia amewatumia maelekezo ya kutengeneza bomu kwa kupitia maongezi yake kwenye mtandao.

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani katika mkoa wa North Rhine-Westphalia ambako ndiko uliko mji wa Essen amekataa kuzungumzia juu ya taarifa za kuhusika kwa kundi la Dola la Kiislam katika njama hiyo iliozimwa.

Wanaume wawili katika mji wa karibu wa Oberhausen wamekamatwa kuhusiana na tishio hilo.Mmmoja wao alihojiwa baada ya polisi kuipekuwa nyumba moja ilioko mjini.Wa pili alichukuliwa kwa ajili ya kuhojiwa kutoka mkahawa wa mtandao ulioko karibu. Duru za usalama zimeliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kwamba wakati watu hao walikuwa na mawasiliano na mwanamgambo huyo wa Ujerumani wakati alipokuwa nchini Syria hawachukuliwi kama watakuwa washirika wake.

Ujerumani katika wasi wasi

Polizei schließt nach Terrordrohung Einkaufszentrum
Polisi katika ulinzi nje ya kituo cha maduka cha Limbecker Platz mjini Essen.Picha: picture alliance/dpa/B. Thissen

Kwa mujibu wa mtandao wake kituo cha maduka cha Limbecker Platz kina zaidi ya maduka 200 na huvutia watu hadi 60,000 katika siku za Jumamosi.

Ujerumani imekuwa katika wasi wasi kufuatia mfululizo wa mashambulizi mwaka jana ikiwa ni pamoja na lile la mhamiaji wa Tunisia aliyekataliwa hifadhi nchini alipowaponda watu waliokuwa katika soko la Krismasi kwa kutumia lori na kuuwa watu 12 mwezi wa Disemba mwaka jana.

Mwezi wa Julai mwaka jana Mjerumani mwenye asili ya Iran ambaye  polisi imesema alikuwa na shauku ya kufanya mauaji ya watu wengi alipowauwa kwa kupiga risasi watu tisa katika kituo cha maduka cha Munich kabla ya kujipiga risasi yeye mwenyewe.

Kundi la Dola la Kiislamu lilidai kuhusika na mashambulizi hayo ya Ujerumani mwaka jana likiwemo lile la kuuwawa kwa kijana mdogo mjini Hamburg,mripuko wa kujitowaq muhanga huko Ansbach na watu kupigwa mashoka kwenye treni huko Würzburg shambulio ambalo limejeruhi watu watano.

Mwandishi : Mohamed Dahman /AFP/AP/dpa /Reuters/DW

Mhariri :Hamidou Oumilkheir