1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake na wasichana 60 waliotekwa nyara na Boko Haram watoroka

Admin.WagnerD7 Julai 2014

Zaidi ya wanawake na wasichana 60 waliokuwa wametekwa nyara na kundi la waasi wenye itikadi kali la Boko Haram kaskazini mwa Nigeria wamefanikiwa kutoroka huku viongozi wa Chiboka wakitaka ulinzi kutoka umoja wa Mataifa

https://p.dw.com/p/1CXQg
Picha: picture alliance/abaca

Mwenyekiti wa serikali za mitaa wa Chibok Pogu Bitrus amethibitisha leo kuwa wanawake na wasichana takriban 60 waliweza kutoroka kutoka mikononi mwa Boko Haram kati ya siku ya Alhamisi na Ijumma wiki iliyopita.

Bitrus amesema amewatuma wajumbe waliokutana na baadhi ya wanawake hao waliofanikiwa kutoroka pamoja na familia zao katika hospitali ya Lassa waliko hivi sasa katika mji jitrani wa Damboa.

Kutoroka kwa wanawake kwathibitishwa

Kiongozi wa makundi ya vijana wanaoshika doria katika mji wa Maiduguri ambao ni mji mkuu wa jimbo la Borno Abbas Gava amesema amefahamishwa kuwa wanawake na wasichana 63 walitoroka wakati watekaji nyara wao walipokuwa wamekwenda kukabliana na wanajeshi katika shambulizi kubwa lililolenga kambi ya kijeshi na makao makuu ya polisi mjini Damboa.

Kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau
Kiongozi wa Boko Haram Abubakar ShekauPicha: picture alliance/AP Photo

Mzazi mmoja wa msichana ambaye ni miongoni mwa waliotekwa nyara na Boko Haram mwezi Aprili katika eneo la Chibok Malam Ayuba amesema walizipata taarifa hizo za baadhi ya wasichana hao kuweza kutoroka kupitia vyombo vya habari.

Ayuba ambaye alihojiwa na idara ya kihausa ya DW ameiomba serikali ya Rais Goodluck Jonathan kufanya kila iwezalo kuwaokoa mabinti zao kutoka mikononi mwa Boko Haram

Kushindwa kwa serikali ya Nigeria kuwaokoa wasichana zaidi ya mia mbili wa shule waliotekwa nyara miezi mitatu kumeibua shutuma kali ndani na nje ya Nigeria.

Serikali ya Nigeria yashutumiwa

Boko Haram inataka wapiganaji wake ambao wamefungwa jela kuachiwa huru ili iweze kuwaachia huru wasichana hao.Inasemekana Rais Jonathan amekataa matakwa hayo ya Boko Haram.

Maandamano ya kuishinikiza serikali ya Nigeria kuwaokoa wasichana wa Chibok
Maandamano ya kuishinikiza serikali ya Nigeria kuwaokoa wasichana wa ChibokPicha: picture-alliance/AP Photo

Bitrus amesema mashambulizi yameongezeka Chibok na vijiji vilivyo karibu huku Boko Haram wakividhibiti na kutishia kuviteka vingine zaidi.Vijiji 19 vya eneo hilo la kaskazini mwa Nigeria vinaripotiwa kushambuliwa tangu kutekwa nyara kwa wasichana hao na zaidi ya watu 229 kuuawa huku wengine kiasi ya 100 wakijeruhiwa vibaya.

Chama cha maendeleo cha eneo la Kibaku jina jingine la Chibok kimesema katika asilimia 90 ya visa vya mashambulizi kulitolewa tahadhari ya mapema lakini jeshi halijaweza kuyatibua mashambulizi hayo.

Chama hicho kimeutaka Umoja wa Mataifa kutumia nguvu zake kuwasaidia na kuwalinda kwani serikali kuu inaonekana kushindwa au kutokuwa na nia ya kuwalinda watu wa eneo hilo na mali zao.

Mwandishi:Caro Robi/ap/dpa

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman