1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake wadhalilishwa kingono Somalia

Mjahida8 Septemba 2014

Shirika la kutetea haki za binaadamu limesema, wanajeshi wa Umoja wa Afrika wanaolinda amani nchini Somalia wamewadhalilisha kingono wasichana na wanawake wa kisomali wanaoishi katika mazingira magumu mjini Mogadishu.

https://p.dw.com/p/1D8hb
Mwanamke Mjini Mogadishu
Mwanamke Mjini MogadishuPicha: Tobin Jones/AFP/Getty Images

Shirika hilo la Human Rights Watch limesema nchi za kiafrika zinazochangia wanajeshi hao pamoja na wafadhili wa AMISOM wanapaswa kushughulikia ukiukaji huo wa haki za binaadamu haraka iwezekanavyo na kuimarisha uataratibu ndani ya Somalia ya kutafuta haki ya wanawake hao.

Ripoti hiyo yenye kurasa 71 na iliopewa jina la “‘The Power These Men Have Over Us' yaani nguvu wanaume hawa walizonazo dhidi yetu, inaonesha wazi visa walivyofanya wanajeshi hao kwa kutumia misaada ya kibinaadamu kwa kuwadhalilisha kingono wanawake na wasichana tangu mwaka wa 2013.

Wanawake nchini Somalia
Wanawake nchini SomaliaPicha: picture alliance/dpa

Wanajeshi hao wanasemekana kutumia misaada hiyo ili kuwashinikiza wanawake kushiriki vitendo vya ngono.

Ripoti hiyo imeendelea kufafanua kuwa wanajeshi hao waliwabaka baadhi ya wanawake waliokuwa wakitafuta msaada wa matibabu pamoja na maji katika kambi za AMISOM.

Kwa mfano mwaka wa 2013 kijana Qamar R ambalo sio jina lake la kweli aliye na Umri wa miaka 15, alikwenda katika eneo wanalokaa wanajeshi wa burundi katika kambi ya AMISOM kuomba usaidizi wa dawa, kwa ajili ya mamake aliyekuwa mgonjwa, baadaye mkalimani wa kisomali akamuamuru kuwafuata wanajeshi wawili waliokuwa na dawa hizo, Qamar aliliambia shirika la HRW kwamba badala ya kupewa dawa alizoitisha alipelekwa katika maeneo ya misitu na kubakwa na mmoja wa wanajeshi hao, kisha baada ya kitendo akapewa dola kumi na aliyemtendea unyama huo.

HRW limewahoji wanawake 21 waliopitia masaibu hayo

Aidha shirika hilo la kutetea haki za binaadamu la HRW limekusanya data zake kwa kuwafanyia mahojiano wanawake 21 na wasichana ambao wameelezea kubakwa au kudhalilishwa kingono na wanajeshi kutoka Burundi na Uganda wanaofanyakazi na wanajeshi wa Umoja wa Afrika.

“Baadhi ya wanajeshi wa Umoja wa Afrika wanatumia nafasi zao vibaya kwa kuwafanyia maovu wanawake na wasichana mjini Mogadishu,” alisema Liesl Gerntholtz, Mkurugenzi wa haki za wanawake katika shirika hilo la HRW.

Gerntholtz amesema Kwa sasa Somalia ina matatizo mengi lakini Uongozi wa Somalia na Umoja wa Afrika unaweza kubadilisha hali ilivyo kwa kuwawajibisha wanajeshi waliotekeleza vitendo vya udhalilishaji wa kingono.

Nembo ya shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch
Nembo ya shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch

Miaka mingi ya mapigano na ukosefu wa chakula nchini Somalia, yamesababisha maelfu ya watu kuyahama makaazi yao, na bila ya kazi au kipato chochote cha kumudu maisha, wengi wanategemea usaidizi kutoka nje na wanalazimika kushawishika katika visa vya udhalilishaji ili kujikimu kimaisha pamoja na watoto wao.

Itakumbukwa kwamba mwaka wa 2007 Baraza la usalama la amani la Umoja wa mataifa liliwapeleka wanajeshi wa kulinda amani nchini Somalia wanaojulikana kama AMISOM chini ya matakwa ya baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulinda miundo mbinu ya Somalia, pamoja na maafisa wa serikali na pia kusaidia katika kutoa misaada ya kibinaadamu.

AU yaombwa kuingilia kati na kusitisha maovu ndani ya AMISOM

Tangu wakati huo majukumu ya wanajeshi hao pamoja na uwepo wao uliongezeka maradufu katika nchi hiyo ya pembe ya Afrika. Wanajeshi wa AMISOM wanachangiwa na mataifa ya Uganda, Burundi, Kenya, Ethiopia, Djibouti, na Sierra Leone.

Hata hivyo wanaharakati wanasema Umoja wa Afrika hauwezi kulifungia jicho suala hili maana ya kwamba watakuwa wanaipoteze4a uaminifu umoja huo katika misheni yake ya kulinda amani Somalia.

Baadhi ya wanajeshi wa kulinda amani wa AMISOM
Baadhi ya wanajeshi wa kulinda amani wa AMISOMPicha: STUART PRICE/AFP/Getty Images

Sasa hivi kinachohitajika ni serikali zinazounga mkono uwepo wa vikosi vya AMISOM zinapaswa kufanya kazi na Umoja wa Afrika kumaliza visa vya udhalilishaji wa kingono kwa wasichana na wanawake nchini Somalia na kuchukua hatua kwa wanajeshi wanaosemekana kutekeleza hujuma hiyo, huku wakifanya kila wawezalo kusimamisha kabisa visa hivyo.

Mwandishi: Amina Abubakar/HRW

Mhariri: Yusuf Saumu