1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake Zimbabwe wataka usawa wa kijinsia

28 Juni 2013

Wakati Zimbabwe ikielekea katika uchaguzi mkuu mwezi ujao, Umoja wa wanawake unaounga mkono mambo ya siasa WiPSU, umezindua Kura kwa kampeni ya mwanamke ili kuongeza idadi ya wanawake katika utungaji wa sera na maamuzi

https://p.dw.com/p/18yGw
Wanawake Zimbabwe
Wanawake ZimbabwePicha: AFP/Getty Images

Akiongea na shirika la habari la IPS mkurugenzi wa umoja huo, Fanny Chirisa amesema kura hiyo kwa ajili ya kampeni ya wanawake, itaongeza idadi ya nafasi za wanawake bungeni na katika serikali ndogo.

Fanny Chirisa amesema mpango huo utaongeza uelewa na muamko katika umma kuwapigia kura wanawake kwa matarajio ya kuwa wanawake hao katika bunge wataboresha maisha ya wanawake wenzao walio ngazi ya chini

Aidha kampeni hiyo pia inalenga kuisaidia Zimbabwe kuleta usawa wa kijinsia, ikiwa ni kwa mujibu wa itifaki ya mpango wa maendeleo ya kijinsia wa nchi za Kusini mwa Afrika.

Itifaki hiyo inajumuisha maendeleo ya vifungu kadhaa na malengo 23, ikiwemo lengo la wanawake nchini humo kufikia asilimia 50 katika nafasi za maamuzi za sekta za umma na binafsi hadi kufikia mwaka 2015. Wanawake nchini humo ni milioni 6-7 kati ya wakaazi wote milioni 12.9 wa Zimbabwe

Akizungumza na shirika la habari la IPS Meneja mipango Marlene Sigauke wa kituo cha Afrika kwa ajili ya kutetea wanawake, shirika ambalo linafanya kazi kwa ajili ya maendeleo ya wanawake Afrika amesema, ili kuleta usawa wa kijinsia sera na ilani za chama cha siasa, zinatakiwa kutekelezwa kwa vitendo.

Marlene Siuake amesisitiza wanawake walioko katika madaraka wanatakiwa kuendeleza hisia za sera hizo ambazo zitawanufaisha wanawake waliopo katika ngazi za chini.

Kwa upande wake naibu waziri wizara ya kazi na ustawi wa jamii Monica Mutsvangwa ameliambia shirika la habari la IPS ni muda sasa kwa wanawake kupambana na haki zao.''Katiba mpya imeweka viti kwa ajili ya wanawake, tunatakiwa kuitumia fursa hiii kuimarisha ustawi wa wanawake'' amesema Monica Mutsvangwa

Mbali na hilo amesema katiba ya nchi hiyo imeweke viti 60 vya usawa wa kijinsia kwa ajili ya wanawake katika sehemu zote mbili, katika viti vya bunge 210 na viti 88 katika baraza la seneti.

Hata hivyo Monica amesema kwa sasas katiba ya Zimbabwe imeweka nafasi 18 za upendeleo kwa wanawake kushiriki katika siasa na hivyo wanawake wanatumia fursa hiyo ya kikatiba kutetekeleza sera hizo na kuziweka katika vitendo

Kwa upande wake mbunge na mwenyekiti wa taifa wa chama cha wanawake bungeni Beaztrice Nyamupinga ameliambia shirika la habari la IPS licha ya Zimbabwe kusaini makubaliano hayo lakini serikali imeshindwa kutekeleza sera hizo.

Nyamupinga amesema wahanga wengi hasa wajane ambao hawaruhusiwi kuwarithi wanaume zao, wanahofia kuripoti matatizo yao kwa hofu ya kuhukumiwa au kuhojiwa na mamlaka au polisi nchini humo.

Amessema katiba mpya ina vifungu vinavyoelezea usawa wa kijinsia na vifungu kadhaa vinavyolinda haki ya wanawake, akiongeza ikiwa wanawake wenyewe hawatakuwa na uakilishi bungeni ili kuhakikisha sheria hizo zinatakelezwa, basi vifungu hivyo kamwe havitafanyiwa kazi.

Wajane wengi nchini Zimbawe wanafukuzwa kutoka katika nyumba za waume wao, baada ya kufariki, kutokana na misimamo mikali ya ndugu za waume zao na ufinyu wa elimu ya kuwalinda wanawake kutoka jeshi la polisi

Maude Taruvinga (mjane) anasema ikiwa atapiga kura katika uchaguzi ujao mwaka huu, atampigia mwanasiasa wa kike wa eneo hilo akiwa na matumani ya mustakabali mzuri kutokana na kuongezeka idadi ya wanawake katika bunge la nchi hiyo.

Mwezi Januari 2012 Maude Taruvinga, alikuwa muathirika wa mfumo-dume wa tamaduni za Zimbabwe wakati wakwe zake walipomtaka kutoka katika nyumba ya mume wake eneo la Marondera Mashariki ya mkoa wa Mashonaland baada ya mume wake kufariki.

Mwandishi: Hashimu Gulana/IPS

Mhariri: Yusuf Saumu