1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanne wafa machafuko ya Cairo

6 Desemba 2012

Vifaru ya kijeshi vimetumwa nje ya Ikulu ya Misri kuzima ghasia zilizoibuka baina ya wafuasi wa Rais Mohammed Mursi na wapinzani wake, ambapo watu wanne wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa kwenye mapigano ya usiku kucha

https://p.dw.com/p/16wW3
Mandamano nchini Misri
Mandamano nchini MisriPicha: Reuters

Vyombo vya habari vimemnukuu Waziri wa Afya wa Misri akisema kuwa watu hao wameuawa kutokana na vurugu zilizozuka nje ya Ikulu ya nchi hiyo ambapo waandamanaji wa upinzani walikuwa wameweka mahema tangu siku ya Jumanne kulalamikia amri iliyomlimbikizia rais madaraka mengi pamoja na uamuzi wake wa kuharakisha katiba.

Kwa mujibu wa taarifa zilizonukuliwa na kituo cha televisheni cha Aljazeera kutoka kwa waziri huyo wa afya, kiasi ya watu 350 wamejeruhiwa wakati waandamanaji waliporushiana mawe na mabomu ya petroli. Mapigano yaliendelea usiku kucha wa kuamkia leo hadi serikali ilipoamua kupeleka vifaru na askari wenye silaha kudhibiti vurugu hizo nje ya Ikulu mapema asubuhi.

Polisi wa kupambana na ghasia walipelekwa kwenye eneo hilo ili kusitisha mapigano hayo lakini bado hali iliendelea kuwa mbaya. Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri watu 32 wamekamatwa hadi sasa katika maandamano hayo ambayo yameenea pia kwenye miji mingine ya nchi hiyo.

Makamo wa Rais asaka suluhu

Ghasia hizo kali zilizoanza tangu jana zilizuka baada ya makamu wa rais wa Misri Mahmoud Mekky kusema marekebisho ya vipengele vyenye utata katika rasimu ya katiba huenda yakajadiliwa na upinzani kabla ya kura ya maoni ya Desemba 15, na kuwekwa katika maandishi.

Wafuasi wa Rais Mohamed Mursi wakipambana na wapinzani wao mjini Cairo.
Wafuasi wa Rais Mohamed Mursi wakipambana na wapinzani wao mjini Cairo.Picha: picture-alliance/dpa

Wakaazi wa jirani na eneo la Ikulu wamekasirika kuona kuwa polisi wamekaa kando na hawafanyi lolote kuwadhibiti waandamanaji kwenye mitaa ambayo walikuwa wanachoma moto vitu mbalimbali. Wapinzani wa Rais Mursi walisikika na kauli mbiu yao inayosema "No to dictatorship" wakiwa na maana ya "hapana kwa udikteta" huku wafuasi wa kiongozi huyo walisikika wakisema "Defending Mursi is defending Islam" wakiwa na maana kuwa kumlinda Mursi ni kuulinda Uislamu.

Marekani ina wasiwasi na hali ya usalama nchini humo na kutaka kufanyika kwa majadiliano ya amani. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, amewaomba Wamisri kuheshimu ahadi yao ya demokrasia.

Vurugu hizo zinatajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kutokea nchini Misri tangu Rais Mursi achukua hatamu ya uongozi katika kipindi kisichofika miezi sita. Taarifa kutoka Ikulu zinasema huenda leo Rais Mursi akatoa tamko hapo baadae. Hapo kabla wapinzani wake walimtaka kuhutubia taifa ili kusaidia kutuliza vurugu na machafuko hayo.

Mwandishi: Stumai George/Reuters/AFP/ DPA
Mhariri: Mohammed Khelef