1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalastina wajipatia serikali ya umoja wa taifa

Oummilkheir15 Machi 2007

Waziri mkuu Ismael Hanniyeh amkabidhi rais Mahmoud Abbas orodha ya baraza jipya la mawaziri

https://p.dw.com/p/CB5E
Rais Mahmoud Abbas na waziri mkuu mteule Ismael Haniyeh
Rais Mahmoud Abbas na waziri mkuu mteule Ismael HaniyehPicha: AP

Waziri mkuu mteule wa Palastina Ismael Haniyah amemkabidhi rais wa utawala wa ndani wa Palastina orodha rasmi ya majina ya mawaziri wa sserikali ya umoja wa taifa baada ya majadiliano tete na ya muda mrefu yaliyolengwa kumaliza mvutano wa ndani na kurejesha imani ya nchi za magharibi.

“Nimemkabidhi rais Mahmoud Abbas orodha ya majina ya mawaziri wa serikali ya umoja wa taifa na amesha iidhinisha”-amesema Ismael Hanniyah mbele ya waandishi habari mjini Gaza.

“Ujumbe wangu kwa wapalastina wote,walio huku nyumbani na walio nchi za nje:tumesuluhisha matatizo yote kuhusiana na serikali ya umoja wa taifa-na hata kuhusu nani anastahiki kua waziri wa mambo ya ndani.”Amesisitiza waziri mkuu huyo mteule.

Kwa mujibu wa msemaji wa kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina,Nabil Abou Roudeina,Mahmoud Abbas ameidhinisha orodha ya mawaziri 25,akiwemo pia waziri mkuu Ismael Hanniyah.

Chama cha Hamas kinawakilishwa na zaidi ya mawaziri kumi serikalini huku Fatah cha rais Mahmoud Abbas wamekabidhiwa wizara sita.

Wizara ya ndani iliyokua chanzo cha mivutano kati ya Hamas na Fatah, amekabidhiwa mwanasiasa anaejitegemea,Hani Al Qawasmeh.Hata wizara ya mambo ya nchi za nje amekabidhiwa mwanasiasa asieelemea upande wowote,Ziad Abou Amr,huku Salam Fayyad wa chama cha “Chaguo la tatu” amekabidhiwa wizara ya fedha.

Baraza hili jipya la mawaziri linakabiliwa na kazi ngumu ya kumaliza mzozo wa ndani wa kisiasa na kurejesha imani ya nchi za magharibi zilizozuwia misaada ya fedha tangu Hamas walipoibuka na ushindi wa uchaguzi wa January mwaka jana na kuunda serikali miezi miwili baadae.

Muakilishi mkuu wa siasa ya nje ya Umoja wa Ulaya Javier Solana,akiwa Nüremberg,kusini mashariki ya Ujerumani,amesema tunanukuu: “Kama tusemavyo kila kwa mara tutasubiri kwanza kuangalia hali ya mambo”Mwisho wa kumnukuu Javier Solana.

Bunge la Palastina litakutana kwa dharura jumamosi ijayo kuliidhinisha baraza hilo jipya la mawaziri.Waziri mkuu mteule Ismael Hanniyeh atachambua baadae muongozo wa serikali yake.,kabla ya kuapishwa mbele ya rais Mahmoud Abbas.

Nakala ya muongozo huo iliyolifikia shirika la habari la faransa AFP inaonyesha serikali hiyo mpya ya Palastina imedhamiria kutuliza hofu za nchi za magharibi kwa akuahidi “kuheshimu maazimio ya kimataifa na makubaliano yaliyotiwa saini na chama cha ukombozi wa Palastina-muongozo huo lakini haukutaja juu ya kutambuliwa dola ya Israel.

Msemaji wa serikali ya Israel Miri Eisin ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP msimamo wa serikali yao haujabadilika-“Hatutaitambua serikali hiyo na wala hatutajadiliana nayo” amesisitiza.

Umoja wa Ulaya na mataifa mengine yanayounda tume ya pande nne inayosimamia utaratibu wa amani ya mashariki ya kati,ambazo ni pamoja na Marekani,Urusi na Umoja wa mataifa wanashurutisha misaada yao kwa serikali ya palastina na kutambuliwa haki ya kuwepo dola ya Israel,Hamas kuachilia mbali matumizi ya nguvu na kuheshimu makubaliano yote yaliyofikiwa miaka ya nyuma.