1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina kutojiingiza kijeshi Syria

10 Aprili 2015

Chama cha Ukombozi wa Palestina PLO kimesema hakitokubali kutumbukizwa katika hatua ya kijeshi kwenye mapambano yanayoendelea katika kambi ya wakimbizi wa Kipalestina nchini Syria.

https://p.dw.com/p/1F66W
Wakimbizi katika kambi ya Yarmouk ,Syria.
Wakimbizi katika kambi ya Yarmouk ,Syria.Picha: Rami al-Sayed for unrwa.org

Mjumbe wa Chama cha Ukombozi wa Palestina mjini Damascus Ahmad Majdalani hapo jana alitowa kauli ambayo inakwenda kinyume na msimamo wa muda mrefu wa Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Wapalestina kwamba Wapalestina hawapaswi kujiingiza katika mzozo wa Syria.

Haikuweza kufahamika mara moja kwa nini Majdlani ambaye alitumwa Damascus mji mkuu wa Syria kuzungumzia suala la mzozo wa kambi ya wakimbizi wa Kipalestina ya Yarmouk ilioko kwenye mji huo amekuja kuunga mkono kujihusisha kijeshi kwa Wapalestina nchini Syria.

Hatua ya kijeshi ni maangamizi

Wasel Abu Youssef afisa mwandamizi wa chama cha PLO amesema leo hii kwamba kinachofaa ni kuzungumzia namna ya kuwaondowa kwa salama waakaazi waliozingirwa wa kambi hiyo badala ya kuchukuliwa kwa hatua ya kijeshi.

Hali katika kambi ya Yarmouk.
Hali katika kambi ya Yarmouk.Picha: picture-alliance/epa/Y. Badawi

Amekaririwa akisema kwamba wanajuwa iwapo jeshi la Syria na ndege zake na vifaru vyake vitaingilia kati jambo hilo litamaanisha kuangamizwa kabisa kwa kambi hiyo.

Wapiganaji wa Dola la Kiislamu waliiteka sehemu kubwa ya kambi hiyo ya Yarmouk wiki iliopita na kutia mguu wao kwa mara ya kwanza katika mji mkuu wa Syria. Kuingia kwa wanamgambo hao ni masahibu mapya kwa waakazi wanaokadiriwa kufikia 18,000 wa kambi ya Yarmouk ambao tayari wamekuwa wakiteseka kutokana na kuzingirwa na vikosi vya serikali kwa miaka miwili,njaa na maradhi.

Kambi ya kifo

Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya Umoja wa Mataofa mjini New York Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bana Ki- moon ameieleza kambi hiyo kuwa ni kambi ya kifo.
Ban amesema "Katika hali yenye kutisha ambayo ni Syria,kambi ya wakimbizi ya Yarmouk ni mkondo wa motoni wa kina kirefu.Baada ya miaka miwili ya kuzingirwa,wakimbizi 18,000 wa Kipalestina na Wasyria hivi sasa wanashikiliwa mateka na wanamgambo wa Dola la Kiislamu na wengine wenye itikadi kali.Kambi hiyo ya wakimbizi inaanza kufanana na kambi ya kifo"

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon.Picha: picture-alliance/dpa/Karim Kadim

Waandishi walioitembelea kambi hiyo hapo Alhamisi wakisindikizwa na vikosi vya serikali wameshuhudia majengo yalioripuliwa yakiwa matupu na barabara zikiwa tupu zilizojaa vumbi.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/

Mhariri: Mohammed Abdul-rahman