1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina waghadhabishwa na Hotuba ya Netanyahu

Saumu Ramadhani Yusuf25 Mei 2011

Rais wa Mamlaka ya Wapalestina, Mahmoud Abbas, ameipinga vikali hotuba ya jana ya waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, mbele ya bunge la Marekani,

https://p.dw.com/p/11O2l
Rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina Mahmoud AbbasPicha: AP

Rais Abbas anasema Wapalestina watasonga mbele na mpango wao wa kutafuta kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa katika kujitangazia dola lao. Mahmoud Abbas anasema hotuba ya Netanyahu ilikuwa na kasoro nyingi na ya kupotosha na imeonyesha wazi kwamba kuna kibarua kigumu cha kufikia amani ya kweli kati ya pande hizo mbili.

Rais wa Palestina Mahmoud Abbas ameonekana mwenye kughadhabishwa na hotuba hiyo ya waziri mkuu wa Israel benjamin Netanyahu iliyoweka wazi msimamo wa taifa hilo la kiyahudi wa kukataa kugawanywa kwa mji wa Jerusalem, suala la kuwarudisha wakimbizi wa Kipalestina na uwezekano wa suala la mipaka ya kabla mwaka 1967 kuwa msingi wa mazungumzo ya kutafuta amani.

Mbele ya macho ya Wapalestina, kwa mujibu wa rais Abbas, waziri mkuu Netanyahu hakuzungumza chochote kinachoweza kuitwa kizuri bali walivyofahamu Wapalestina ni kwamba tayari Netanyahu ameshapitisha uamuzi juu ya matokeo ya hatima ya masuala yote ya msingi katika mgogoro huo bila hata ya kufanyika mazungumzo.

Msimamo wa Wapalestina

Kutokana na hali hiyo, rais Abbas amesisitiza kwamba ikiwa hakuna hatua itakayopigwa kabla ya mwezi Septemba, msimamo wao ni kulifikisha suala hilo katika Umoja wa Mataifa. Nabil Shaath, afisa wa ngazi ya juu ndani ya chama cha rais Abbas cha Fatah, anasema utawala wa Palestina umeshaamua kwamba hatua itakayofuata ni kufanya kile walichokifanya Waisraeli mwaka 1948, na kisha kwenda Umoja wa Mataifa kutaka kutambuliwa. Ameendelea kuikosoa hotuba ya Netanyahu, akisema:

"Nadhani hakuna pendekezo la amani lililotolewa katika hotuba hii, bali ni hotuba iliyozungumzia vita zaidi kuliko amani. Alichokifanya Netanyahu ni kuzungumzia tu historia ya kutokuwepo haki na kukataa kutambua haki zetu ndani ya adhi yetu. Amezungumzia tu haki ya watu kurudi katika nchi yao wanayodai ilikuwa yao kwa miaka 4000, lakini ikawa ni jambo lisilowezekana kwa wakimbizi wakiüpalestina waliofurushwa kutoka katika ardhi yao miaka 60 iliyopita kurudi majumbani kwao''.

Israel yataka kutambuliwa kama taifa la Kiyahudi

Aidha mapema hii leo mpatanishi wa Palestina, Saeb Erakat, aliwaambia waandishi wa habari kwamba hotuba ya waziri mkuu Netanyahu imeonyesha wazi kwamba serikali hiyo ya Israel sio mshirika katika mchakato wa amani na kuongeza kusema kwamba Wapalestina hawawezi Kuitambua Israel kama dola la Kiyahudi.Na kusema,

''Bwana Netanyahu hapaswi hata mara moja kufikiria juu ya suala hili, wakati kuna Waarabu wapatao millioni 1.5 ambao sio Wayahudi wanaoishi ndani ya Israel. Anawezaje kuzungumzia juu ya taifa la Kiyahudi?''

Kukwama kwa Mazungumzo

Mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina yamekwama tangu mwezi Septemba mwaka jana kufuatia mvutano juu ya hatua ya Israel ya kuendeleza ujenzi wa makaazi ya walowez,i mpango uliotangazwa muda mfupi baada ya mazungumzo hayo kuanzishwa upya mjini Washington. Hadi sasa Netanyahu amekataa kusimamisha hatua hiyo, na Wapalestina wanasema hawarudi katika meza ya mazungumz ya amani hadi ujenzi utakapositishwa. Na juu ya hilo, endapo mazungumzo yatashindwa kurudi, Wapalestina wataendelea na mpango wao wa kwenda Umoja wa Mataifa kutaka kutambuliwa. Rais Obama lakini ameshatangaza wazi msimamo wake juu ya hatua hiyo akisema haiungi mkono.

Mwandishi Saumu Mwasimba/DPAE

Mhariri Othman Miraji