1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina wajibu mashambulizi ya Israel

23 Machi 2011

Kundi la wapiganaji wa Kiislamu la Jihad la Palestina limerusha maroketi katika miji ya Israel ya Beersheba na Ashdod, kulipiza kisasi mashambulizi ya Israel ambayo hadi sasa yameshaua Wapalestina tisa.

https://p.dw.com/p/10g79
Mabaki ya kambi ya Hamas, baada ya mashambulizi ya Israel
Mabaki ya kambi ya Hamas, baada ya mashambulizi ya IsraelPicha: picture-alliance/dpa

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa kitengo cha kijeshi cha kundi la Hamas cha Al-Qassam Brigades, Abu Obeid, imeeleza kuwa mashambulizi hayo ni sehemu ya majibu kwa Israel kutokana na mashambulizi inayoyafanya dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.

Msemaji wa jeshi la Israel, amesema kuwa shambulio la roketi la leo asubuhi lililenga katika mji wa Beersheba uliopo kusini mwa nchi hiyo na kumjeruhi mtu mmoja.

Kwa upande wa Palestina, mwanamgambo mmoja ameuwawa katika mashambulizi ya anga ya leo (23.03.2011) ya Israel. Kwa mujibu wa msemaji huyo, jana jioni shambulio jingine la roketi lilifanywa kutoka Ukanda wa Gaza kwenda katika mji wa Ashdod, lakini likitua upande wa kusini.

Jeshi la Israel limebainisha kuwa, jana wanamgambo wa Gaza walifanya mashambulizi tisa ya roketi kwenda Israel, pamoja na kufyatua makombora saba.

Mwishoni mwa wiki iliyopita wanamgambo walivurumisha makombora 50 kwenda kusini mwa Israel.

Mashambulizi hayo ya hivi karibuni yanafuatia kuibuka kwa ghasia za mpaka ambazo zimesababisha wasiwasi kati ya Israel na kundi la Hamas la Gaza, hivyo kuzusha hofu ya uwezekano wa Israel kulivamia kijeshi eneo hilo.

Ban Ki-moon alaani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moonPicha: dapd

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amelaani vikali mauaji ya Wapalestina wanane, wakiwemo watoto wawili katika Ukanda wa Gaza ambayo yamefanywa na vikosi vya Israel.

Katika taarifa yake, Bwana Ban amesema ana wasiwasi sana kuhusu hali kuzidi kuwa mbaya huko Gaza na kusini mwa Israel na kutoa wito kwa pande zote kuheshimu majukumu yao kwa kuzingatia sheria za kimataifa.

Pia katibu huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani mashambulizi ya roketi yaliyofanywa na makundi ya wanamgambo wa Kipalestina.

Hamas imekuwa ikirusha roketi katika siku za hivi karibuni ikiilenga Israel jambo lililoifanya nchi hiyo nayo kujibu kwa kufanya mashambulizi ya anga na ardhini.

Haniya ataka Baraza la Usalama kuingilia kati

Wapiganaji wa Hamas
Wapiganaji wa HamasPicha: AP

Waziri Mkuu wa serikali ya kundi la Hamas inayodhibiti Ukanda wa Gaza, Ismail Haniya, amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za kuwalinda watu wa Gaza na kuiadhibu Israel.

Aidha, kwa upande mwingine, kiongozi wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas ambaye kwa sasa yuko Moscow, Urusi, amelaani mashambulizi hayo ya Israel yaliyoangamiza maisha ya Wapalestina, wakiwemo watoto.

Naye Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ameelezea masikitiko yake kutokana na mauaji hayo, lakini amesisitiza kuwa mashambulizi hayo yalifanyika katika kujibu mashambulizi mengine yaliyofanywa na Hamas kwa raia wa Israel.

Mashambulizi haya ni makubwa kufanyika tangu vita vya Gaza vya siku 22 ambavyo vilianza mwishoni mwa Desemba mwaka 2008 na kumalizika Januari mwaka 2009.

Katika vita hivyo, Wapalestina 1,400 waliuwawa, zaidi ya nusu wakiwa ni raia ambapo pia Waisrael 13 waliuawa, 10 kati yao wakiwa ni wanajeshi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)
Mhariri: Josephat Charo