1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina wakubaliana kumaliza mivutano

Saumu Mwasimba
10 Februari 2021

Vyama vya Fatah na Hamas pamoja na makundi mengine ya Wapaestina wameridhia juu ya kuandaliwa uchaguzi wa bunge na rais na kuafikiana kuyaheshimu matokeo yatakayotokana na chaguzi hizo

https://p.dw.com/p/3p9cj
Ägypten Treffen zwischen Hamas und Fatah in Kairo
Picha: REUTERS

Wapalestina kutoka pande zinazohasimiana wamekubaliana kuhusu hatua za kuhakikisha uchaguzi utafanyika kama ilivyopangwa baadae mwaka huu. Viongozi wa chama cha Fatah na Hamas wamekubaliana  kwa pamoja kuyaheshimu matokeo ya uchaguzi utakaofanyika kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 15.

Ni maazimio yaliyotokana na kikao kirefu cha mazungumzo ya siku mbili mjini Cairo-Misri kati ya wajumbe wa chama cha Fatah kinachoshikilia madaraka Ukingo wa Magharibi na kile cha Hamas kinachodhibiti madaraka ya Ukanda wa Gaza.Taarifa ya pamoja iliyofuatia mazungumzo hayo iliyotolewa jana Jumanne imeeleza kwamba pande zote mbili pamoja na makundi mingine  12 vya Palestina wameridhia kuweka kando tafauti zao na kuandaa uchaguzi kama ilivyopangwa baadae mwaka huu,ikiwemo kundi la wanamgambo wa itikadi kali la Islamic Jihad. Wote kwa pamoja wameahidi kufuata ratiba ya uchaguzi na kuheshimu na kuyakubali matokeo. Msimamo huu uliotoka kwenye mkutano wa Cairo umekuja kufuatia kuwepo shakashaka nyingi kuhusu ikiwa kweli uchaguzi huo utafanyika. Lakini shaka shaka hizo huenda zimepatiwa jibu kwenye mkutano huo kama ambavyo amesikika akisema afisa mwandamizi kutoka chama cha Fatah Jobril Rajoub

Palästinenserführer Abbas feiert Wahlsieg
Picha: AP

"Na leo tumetengeneza mpango tutakaouzingatia na nawaambia Wapalestina kuwa na imani na kile tulichokubaliana,tuamini kwamba mazungumzo yetu yalizingatia mambo mawili,kwanza ni kulinda maslahi yetu na haki zetu na malengo yetu na pili ni kujenga  mfumo wa utaratibu ambao utatusaidia kufikia malengo na ndoto zetu kuelekea hatua ya kuishi ndani ya dola letu''

Kwa maelezo ya taarifa ya pamoja ni kwamba sasa Wapalestina wameamua kujenga umoja wao badala ya mtengano.Kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh amemshukururais Mahmoud Abbas kwa kuyaunga mkono mazungumzo ya Cairo. Ikumbukwe kwamba Wapalestina kwa kipindi cha miaka 15 wameshindwa kufanya uchaguzi sio Ukingo wa Magharibi,Gaza wala Mashariki mwa Jerusalem,kutokana na mpasuko na mvutano mkubwa kati ya chama cha rais Mahmoud Abbas cha Fatah na kile kinachoongozwa na waislamu wenye misimamo mikali Hamas.

Na mazungumzo haya ya mjini Cairo yaliyozikutanisha pande zote yalilenga kufikia makubaliano ya kuandaa chaguzi za bunge mnamo tarehe 22 May na uchaguzi wa rais Julai 31 na azma hiyo imefikiwa.

Westjordanland Wahlen Gerichtshof in Ramallah
Picha: Getty Images/AFP/A. Momani

Kadhalika makundi yote yaliyoshiriki mkutano huo pia yameridhia uundwaji wa mahakama maalum ya uchaguzi ambapo majaji watakaoiendesha mahakama hiyo watatoka katika maeneo yote matatu ya mamlaka ya Palestina kwa maana ya Ukingo wa Magharibi,Gaza na Jerusalem Mashariki.

Mahakama hiyo itakuwa na wajibu wa kutoa uamuzi kuhusu mivutano yoyote ya kisheria kuhusu uchaguzi . Kumbuka kwa ujumla kuna watu milioni 2.8 wenye haki ya kupiga kura Gaza na ukingo wa Magharibi na  mara ya mwisho ulipofanyika uchaguzi wa bunge 2006 matokeo ya ushindi mkubwa wa chama cha Hamas yaliushanga ulimwengu.

Mwandishi:Saumu Mwasimba