1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina wakubaliwa kujiunga na mikataba ya kimataifa

11 Aprili 2014

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameyakinisha maombi ya Wapalestina kujiunga na mikataba 13 ya kimataifa yamezingatia utaratibu sahihi na ameyakubali lakini Israel imekasirika na kuiweka vikwazo Palestina.

https://p.dw.com/p/1BgKv
Rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmud Abbas wakati aliposaini ombi la kujiunga na mashirika ya Umoja wa Mataifa mjini Ramallah Ukingo wa Magharibi. (01.04.2014)
Rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmud Abbas wakati aliposaini ombi la kujiunga na mashirika ya Umoja wa Mataifa mjini Ramallah Ukingo wa Magharibi. (01.04.2014)Picha: Abbas Momani/AFP/Getty Images

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameyakinisha kwamba maombi ya Wapalestina kujiunga na mikataba 13 ya kimataifa yamezingatia utaratibu sahihi na ameyakubali lakini kutokana na hatua hiyo ya Wapalestina, Israel imeweka vikwazo dhidi ya Wapalestina ambavyo vinatowa pigo kubwa kwa mchakato wa amani wa Mashariki ya Kati .

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujaric amewaambia waandishi wa habari hapo jana kwamba Ban ameyajulisha mataifa yote wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa juu ya kukubali kwake maombi hayo.

Baada ya Israel kushindwa kuwaachilia wafungwa wa Kipalestina kulikopangwa siku chache baada ya tarehe ya mwisho waliotakiwa kufanya hivyo mwishoni mwa mwezi wa Machi,Wapalestina walichukuwa hatua ya kulipiza kisasi kwa kusaini baruwa za maombi ya kujiunga na makubaliano 15 ya kimataifa ambapo 15 mashirika yake yako Umoja wa Mataifa moja liko Geneva na jengine liko Uholanzi.

Riyad Mansour balozi wa Wapalestina katika Umoja wa Mataifa amesema mapema wiki hii kwamba Palestina itakuwa mwanachama rasmi wa mikataba 13 kati ya 15 hapo tarehe pili Mei na iko tayari kutuma maombi zaidi ya kujiunga na mashirika ya Umoja wa Mataifa, makubaliano na mikataba kwa kutegemea hatua zinazochukuliwa na Israel.

Vikwazo dhidi ya Wapalestina

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon.Picha: Reuters

Kutokana na hatua hiyo ya Wapalestina,Israel imeanzisha vikwazo dhidi ya Wapalestina na kutowa pigo kubwa kwa mchakato wa amani Mashariki ya Kati ambao tayari unakabiliwa na matatizo.

Israel ambayo hukusanya kodi ya euro milioni 80 sawa na dola milioni 111 kwa niaba ya Mamlaka ya Wapalestina ikiwa ni theluthi mbili ya mapato yake imeamuwa kuzuwiya uhamishaji wa fedha hizo.

Israel pia imesitisha ushiriki wake na Wapalestina katika uendelezaji wa kisima cha gesi nje ya Ukanda wa Gaza na kuweka vikomo kwa akiba za fedha za Wapalestina zilioko kwenye mabenki yake.

Mjumbe mkuu wa usuluhishi wa Wapalestina Saeb Erakat ameishutumu hatua hiyo na kukiita kitendo hicho kuwa ni utekaji nyara wa Israel na wizi wa fedha za wananchi wa Palestina.

Ameliambia shirika la habari la AFP kwamba uamuzi huo ni ukiukaji wa sheria na kanuni za kimataifa uliofanywa na Israel kulipiza kisasi hatua ya Wapalesina kujiunga na mikataba kadhaa kama taifa.

Tetesi za makubaliano

Msemaji wa waizara ya mambo ya nje ya Marekani Jen Psaki.
Msemaji wa waizara ya mambo ya nje ya Marekani Jen Psaki.Picha: SAUL LOEB/AFP/Getty Images

Awali msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Jen Psaki amethibitisha kuwa duru mpya ya mazungumzo kati ya wapatanishi wa Israel, Wapalestina na Marekani yamefanyika hapo jana lakini hakutilia mkazo repoti kwamba makubaliano yanakaribia kufikiwa.

Amesema tafauti zinapunguwa lakini tetesi zozote kuhusu makubaliano ni mapema mno kuzizungumzia wakati huu.

Mazungumzo hayo yalikwaa kisiki kipya wiki iliopita baada ya Israel kugoma kuliachilia kundi la mwisho la wafungwa wa Kipalestina na Wapalestina kulipiza kisasi kwa kutuma maombi ya kujiunga na mikataba kadhaa ya kimataifa.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ameilaumu Israel wiki hii kwa kukwama kwa mazungumzo hayo wakati serikali ya Marekani ikitafakari muda gani zaidi unahitajika kutumika katika mazungumzo hayo yalioko hatarini kusambaratika.

Mwandishi : Mohamed Dahman AFP/

Mhariri:Yusuf Saumu