1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapatanishi wajadili kurefushwa usitishwaji mapigano Gaza

Bruce Amani
29 Novemba 2023

Wapatanishi wa kimataifa wanaendelea na juhudi za kuurefusha mpango wa kusitishwa mapigano Gaza, wakitumai kuwa watawala wa ukanda huo, Hamas wataendelea kuwaachia huru mateka kwa kubadilishana na wafungwa wa Kipalestina

https://p.dw.com/p/4ZZSC
Mabadilishano ya mateka | Kivuko cha Rafah
Gari la Shirika la Masalaba Mwekundu likiwa limewabeba mateka waliokabidhiwa na Hamas.Picha: Ibraheem Abu Mustafa/REUTERS

Wapatanishi wa kimataifa wanaendelea na juhudi za kuurefusha mpango wa kusitishwa mapigano Gaza, wakitumai kuwa watawala wa ukanda huo, Hamas wataendelea kuwaachia huru mateka kwa kubadilishana na wafungwa wa Kipalestina.

Mpango wa sasa wa usitishwaji mapigano utakamilika kesho. Israel imepongeza hatua ya kuwachiwa kwa makumi ya mateka katika siku za karibuni na inasema itaendelea kusitisha mapigano kama Hamas itaendelea kuwaachia huru mateka.

Soma piaUsitishaji vita waibua matumaini ya mateka zaidi kuachiwa

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Ujasusi la Marekani - CIA William Burns na David Barnea, anayeongoza shirika la ujasusi la Israel, Mossad, wako Qatar kujadili kurefushwa kwa usitishwaji mapigano na kuwachiwa huru mateka zaidi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken anatarajiwa kuzuru kanda hiyo wiki hii, na pia anatarajiwa kushinikiza usitishwaji mapigano kwa muda mrefu.