1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapiga kura wachache walijitokeza katika uchaguzi Kenya

27 Oktoba 2017

Tume ya uchaguzi nchini Kenya IEBC inasema takriban watu milioni 6.5, ndio walioteremka vituoni katika marudio ya uchaguzi wa rais uliosusiwa na muungano mashuhuri wa upande wa upinzani NASA

https://p.dw.com/p/2mbsb
Kenia Wahlen
Picha: picture-alliance/AP Images/S.Abdul Azim

Huku kura zikiendelea kuhesabiwa nchini Kenya, kumeripotiwa idadi ndogo ya wapiga kura walioshiriki katika marudio ya uchaguzi wa rais hapo jana, hii ikiwa theluthi moja ya wapiga kura hao ikilinganishwa na uchaguzi wa awali wa Agosti 8.

Idadi hiyo ilikuwa ya chini sana kuliko asilimia 80 ya wapiga kura walioshiriki kwenye uchaguzi wa awali wa Agosti 8 ambao baadaye ulibatilishwa na mahakama ya juu kufuatia dosari zilizopatikana. Uamuzi huo ulikuwa wa kihistoria barani Afrika.

Kulingana na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Kenya, Wafula Chebukati, hesabu ya kura ni kulingana na matokeo kutoka katika maeneo bunge 267 kati ya 290.

Wafuasi wa upinzani wakimbia wakati wa makabiliano na polisi Kibera
Wafuasi wa upinzani wakimbia wakati wa makabiliano na polisi KiberaPicha: picture-alliance/AP Photo/D.Bandic

Kupitia mtandao wake wa Twitter alisema asilimia 90 ya data kutoka maeneo bunge inaonyesha chini ya asilimia 35 ya wapiga kura millioni 19.6 waliosajiliwa walipiga kura hapo jana.

Amesema kwa sasa wamepokea matokeo kutoka vituo vingi vya kupigia kura isipokuwa asilimia 10 nchini kote.

Uchaguzi waahirishwa katika kaunti 4

Tume hiyo iliahirisha upigaji kura katika kaunti nne ambazo ni ngome za upinzani hadi Jumamosi kwa sababu wafuasi wa upinzani walizuia vituo vya kupigia kura kufunguliwa na kukabiliana na polisi. Katika makabiliano makali na maafisa wa polisi, watu wanne wameripotiwa kuuawa na wengine kujeruhiwa. Chebukati amesema hatua hiyo ni kutokana na changamoto za usalama.

Polisi waliripoti ghasia katika kaunti tano kati ya kaunti 47 za Kenya Aalhamisi.

Rais Kenyatta akipiga picha na mmoja wa wafuasi wake Gatundu
Rais Kenyatta akipiga picha na mmoja wa wafuasi wake GatunduPicha: Reuters/S. Modola

Uamuzi huo umeibua hisia kali kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kidini wanaolenga kufanya ibada yao siku hiyo ya Jumamosi wakisema hilo halitowezekana.

Rais Kenyatta atarajiwa kushinda

Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kushinda pakubwa akikosekana mpinzani wake mkuu Raila Odinga ambaye alisusia kushiriki kwenye uchaguzi huo, hata hivyo uhalali wake unatiliwa shaka kutokana na idadi hiyo ndogo ya wapiga kura.

Rais Uhuru Kenyatta alitangazwa kuwa mshindi kwenye uchaguzi wa agosti huku; kiongozi wa upinzani Raila Odinga, ambaye hatua ya kisheria iliyochukuliwa ilisababisha kura hiyo kufutiliwa mbali, Odinga alijiondoa kwenye uchaguzi mpya, akisema mchakato haukuwa wa kuaminika kwa sababu ya ukosefu wa mageuzi ya uchaguzi.

Mwandishi: Fathiya Omar/AFPE

Mhariri: Gakuba, Daniel