1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapiganaji wa kundi la Islamic Jihad wamefyatua makombora katika upande wa Israel

Scholastica Mazula13 Machi 2008

Wapiganaji wa kundi la Wapalestina la Islamic Jihad wamefyatua makombora katika upande wa Israel kutoka ukanda wa Gaza baada ya Israel kuvamia katika Ukingo wa Magharibi.

https://p.dw.com/p/DNzn
Waziri wa ulinzi wa Israel Ehud Barak, kulia akiwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair, kushoto walipokutana Jerusalem, July 23, 2007.Picha: AP

Machafuko hayo mapya yanatishia juhudi za kufanikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano yanayosimamiwa na Misri. Wakati huohuo Kansela wa Ujerumani Angela Markel anatarajiwa kufanya ziara ya siku tatu nchini Israel.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, hakuna taarifa zozote za watu kujeruhiwa katika mapigano hayo yaliyotokea mpakani katika mji wa Sderot.

Hilo ni shambulio la kwanza kufanywa na wapiganaji wa kundi la Islamic Jihad tangu march tano.

Israel ambayo haikushambulia katika eneo la Ukanda wa Gaza linalomilikiwa na chama cha Hamas, ilifanya mashambulizi ya anga kwa kurusha maroketi hadi katika mji wa Beit Hanoun baada ya mji wa Sderot kuwaka moto.

Wapiganaji hao wa kundi la Islamic Jihad wameamua kulipiza kisasi baada ya majeshi ya Israel kuwaua wafuasi wao wanne jana katika Ukanda wa Gaza.

Tayari Israel imepuuza mwito uliotolewa na chama cha Hamas wa kutaka kufanya mazungumzo ya kumaliza vita katika ukanda huo wa Gaza.

Misri imekua ikifanya juhudi za kusitisha mashambulio ya maroketi ya Hamas ndani ya Israel na juhuma za Israel huko Gaza.

Akizungumzia juhudi hizo Waziri wa ulinzi wa Israel Ehud Barak amesema wako katika hali ya kukubaliana kwamba kila juhudi zinapaswa kufanywa kuzuwia hujuma za maroketi Hayo ya Kassam, ili watu wetu hapa waweze kurudishiwa usalama.

Lakini sambamba na hayo Waziri wa ulinzi wa Israel Ehud Barak amesema pia kwamba kutokana na operesheni hiyo inaonyesha wazi kwamba Israel itaendelea kulipiza kisasi.

Jana Barak alisisitiza kwamba hakukuwa na makubaliano baina ya Israel na Wanachama wa chama cha Hamas na kuonya kwamba Israel itaendelea na mashambulizi endapo makombora ya maroketi yataendelea kuvurumishwa katika ukanda wa Gaza.

Wakati kiongozi wa Chama cha Hamas naye alisisitiza kuwa endapo Israel itaridhia kukomeshwa kwa uvamizi na kuondoa vizuizi vilivyowekwa Gaza, tangu Hamas walipotwaa madaraka kwa nguvu mwezi Juni, wanamgambo wa Kipalestina watakutana kushauriana na kutoa jibu saa kwa ajili ya mpango wa kuweka chini silaha.

Wakati huohuo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anatarajiwa kufanya ziara ya siku tatu nchini Israel.

Hatua hiyo ya Merkel itakuwa ni ya kipekee kwani itadhihirisha kuwa Ujerumani inakubali mchango wake katika mauaji ya wayahudi wakati wa Vita vya dunia.

Balozi wa Israel nchini Ujerumani Yoram Ben-Zeev, ameielezea ziara hiyo kuwa ni moja ya vitu muhimu ambavyo vimekuwa havifanywi na Serikali kwa miaka mingi.

Afisa wa ngazi ya juu wa Serikali ya Ujerumani ameelezea umuhimu wa ziara hiyo ambayo inatarajiwa kuanza Jumapili wiki hii na kwamba imekuja wakati ambao Israel inaadhimisha miaka sitini tangu kuanzishwa kwa Taifa hilo.

Kansela Merkel anatarajiwa kuongozana na Mawaziri wengine saba akiwemo Waziri wa mambo ya nje Frank Walter Steinmeier ambao pamoja na mambo mengine watakwenda pia kufanya mazungumzo na upande mwingine wa upinzani wa Israel.