1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapinzani DRC waitisha maandamano zaidi

Jane Nyingi20 Septemba 2016

Makundi ya upinzani katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yameitisha maandamano mengine ya kumpinga Rais Joseph Kabila, siku moja baada ya makabiliano yanayodaiwa kusababisha vifo vya watu 50.

https://p.dw.com/p/1K5Iv
Demokratische Republik Kongo Protest Opposition in Kinshasa
Picha: Reuters/K. Katombe

Idadi hiyo ya waliofariki inatofautiana na ile iliyotolewa na serikali inayosema ni karibu watu 17 tu waliouawa kufuatia makabiliano hayo mjini Kinshasa kati ya waandamanaji na walinda usalama.

Hali imeendelea kuwa tete nchini Kongo. Usiku wa kuamkia leo, makao makuu ya vyama vitatu vya upinzani yameteketezwa kwa moto. Maiti tatu zilizoungua kabisa kiasi cha kutoweza kutambulika zilitolewa katika jengo la chama kikuu cha upinzani cha Union for Democracy and Social Progress, UDPS, huku watu wengine wawili wakiteketezwa moto wakiwa hai na mwengine mmoja kujeruhiwa.

Mashambulizi hayo ya moto yanatokea baada ya makabiliano ya jana kati ya polisi na waandamanaji katika mji mkuu, Kinshasa. Kwa mujibu wa ripoti za serikali, miongoni mwa waliopoteza maisha kufuatia maandamano hayo ni pamoja na maafisa wanne wa usalama.
Viongozi wa upinzani wanamtaka Rais Kabila, ambaye ameongoza Kongo tangu mwaka 2001, kujiuzulu, wakisema analenga kuongeza muhula mwengine kinyume na katiba. Makabiliano hayo ya jana yametajwa kuwa mabaya zaidi kutokeoa mjini Kinshasa tangu Januari mwaka 2015, baada ya polisi kuyavunja maandamano mengine ya upinzani yaliyosababisha vifo vya watu kadhaa. Waziri wa Usalama wa Ndani, Evariste Boshab, ameyataja maandamano hayo yanayofanywa na upinzani kama maasi na kusema serikali haitayavumilia

Demokratische Republik Kongo Protest Opposition in Kinshasa
Walinda usalama wakikabiliana na waandamanaji mji wa KinshasaPicha: Reuters/K. Katombe

Japo Rais Kabila amezuiwa na katiba kugombea muhula mwingine, hajachukua hatua zozote kutoa ratiba ya kufanyika uchaguzi mkuu, hali iliyozua wasiwasi kuwa huenda akaendelea kukaa madarakani, hata baada ya muda wake kukamilika tarehe 20 mwezi Disemba mwaka huu. Mwandamanaji mmoja alisema hawatamkubalia Rais Kabila tena "Sisi tunazingatia Kifungu cha 64 cha Katiba. Muda wa kuhudumu Kabila umemalizika. Iwapo anataka kutuuwa, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, itamshughulikia. Hatumtaki tena. Anapaswa kuondoka ofisini. Muda wake wa kuhudumu umekamilika. Anapaswa kuondoka."

Kongo Präsident Joseph Kabila
Rais wa DR Kongo Joseph Kabila (Katikati) katika sherehe za kuadhimisha uhuru wa Kongo, eneo la KinduPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Bompengo

Taifa hilo la kati mwa Afrika lenye utajiri wa madini halijawahi kushuhudia amani wakati wa kupokezana madaraka. Waagalizi kutoka mataifa ya magharibi na wafadhili wanahofia huenda vurugu za kisiasa zinazoendelea DRC huenda zikabadilika na kuwa vita katika taifa hilo linalosumbuliwa wa wapiganaji

Mwandishi: Jane Nyingi AFP/RTRE

Mhariri: Mohammed Khelef