1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapinzani Syria kuendeleza mapambano

Admin.WagnerD30 Machi 2012

Wapinzani nchini Syria wameitisha mandamano baada ya swala ya Ijumaa kupinga maazimio ya Jumuiya ya Umoja wa nchi za Kiarabu kuhusu mgogoro wa Syria baada ya Mkutano wao Mjini Baghdad siku ya Jumatano

https://p.dw.com/p/14VBr
Wandamanaji nchini Syria
Wandamanaji nchini SyriaPicha: Edlib News Network ENN/AP

Katika taarifa iiliyowekwa kwenye ukurasa wao wa facebook, wanaharakati hao walisema Waislam na waarabu wamewatelekeza lakini Mwenyezi Mungu yuko pamoja nao na kuongeza kuwa dhamira yao itawaletea ushindi, huku wakihimiza raia kote nchini Syria wajitokeze kwa wingi kushiriki mandamano hayo yanayofanyika kila wiki baada ya swala ya Ijumaa.

Mkutano wa jumuiya hiyo uliomalizika siku ya Jumatano mjini Baghdad nchini Iraq uliidhinisha azimio linaloutaka utawala wa Rais Bashar al Assad kukomesha mauaji na ukandamizaji wa wapinzani, huku ukiwataka wapinzani kuungana na kunazisha mjadala wa kitaifa unaolenga kumaliza tofauti zilizopo.

Ban Ki-Moon, Nabil al Arabi wanena
Katika Mkutano huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon na yule wa Jumuiya ya Umoja wa nchi za Kiarabu Nabil al Arabi walikubaliana kwamba ni muhimu kwa Rais Assad kutekeleza ahadi kwa vitendo.

"Tunaweza kusema matumaini yalikuwepo pale Syria ilipokubaliana na Mpango wa hatua sita. Sasa tunahitaji kuona utekelezaji. Na hilo laazima lifanyike kwa uwazi. Kwa sasa bado halijanyika, lakini Mwenyezi Mungu akipenda tutafanikiwa," alisema Nabil al Arabi

Baadhi ya viongozi wa nchi za kiarabu waliohudhuria Mkutano wa Jumatano
Baadhi ya viongozi wa nchi za kiarabu waliohudhuria Mkutano wa JumatanoPicha: picture-alliance/dpa

Upande wa upinzani ulitaka Mkutano huo utoe tamko zito kama ilivyokuwa inapendekezwa na nchi za Qatar na Saudi Arabia ambazo zilimtaka Rais Assad aachie madaraka na ikishindikana waasi wapatiwe zana za kivita ili wawe na nguvu ya kupambana na vikosi vya serikali kama ilivyofanyika huko Libya.

Ahadi ya Assad
Rais Assad kwa upande wake alisema atafanya kila liwezekanalo kuhakikisha mpango wa mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa nchi za Kiarabu, Koffi Annan, unatekelezwa lakini akataka na waasi wanaopambana na serikali yake nao wasitishe mashambulizi.

Uturuki yazidi kushinikza
Naye Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan akiwa ziarani nchini Iran, aliutaka utawala nchini Syria kuheshimu matakwa ya wanachi na kufanya mageuzi ya kiasiasa ikiwa ni pamoja na kuanda uchaguzi huru na wa haki. Alisema kama Rais Assad haogopi na anauamini utawala wake, basi hana budi kukubali kuundwa kwa vyama vya kisiasa na kuruhusu ushindani.

Waziri Mkuu Tayyip ambaye nchi yake inapakana na Syria kwa upande wa kaskazini aliongeza kuwa endapo rais assad atashinda uchaguzi, basi Uturuki haitakuwa na tatizo lolote na kiongozi huyo. Pia aliiomba Iran ambayo ni mshirika mkubwa wa Syria, ishirikiane na Uturuki kuhakikisha uchaguzi huru unafanyika nchini Syria.

Mgogoro wa Syria ambao unaendelea kwa zaidi ya mwaka moja, umesababisha vifo vya zaidi ya watu 9000 hadi sasa kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa.

Mwandishi: iddi Ismail Ssessanga\AFPE\APE\
Mhariri: Mohamed Abdul Rahman