1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapinzani Syria wapewa siku 15 kujisalimisha

2 Mei 2011

<p>Serikali ya Syria imewapa watu waliotekeleza vitendo vya uvunjaji sheria muda wa siku 15 kujisalimisha katika vyombo vya sheria kote nchini humo.

https://p.dw.com/p/117Za
Waandamanaji wakibeba jeneza la mwenzao aliyeuwawaPicha: picture alliance/dpa
Watu kadhaa wameripotiwa kukamatwa kufuatia wimbi la upinzani dhidi ya serikali. Tangazo hilo la serikali limekuja wakati ambapo wanaharakati wanapanga maandamano mengine dhidi ya serikali kufuatia kuuwawa kwa watu kadhaa katika maandamano ya mwishoni mwa wiki.

Wizara ya mambo ya ndani ya Syria hii leo imetoa tangazo la kuwataka raia wote wa nchi hiyo walioshiriki au kutekeleza visa vya uvunjaji wa sheria kama vile kumiliki silaha kinyume cha sheria, kushambulia vikosi vya usalama au kueneza propaganda za uongo kujisalimisha kwa vyombo vya usalama kufikia tarehe 15 mwezi huu na kuweka chini silaha zao. Aidha serikali imewataka wananchi kutoa taarifa kuwahusu wanaoisaliti serikali, magaidi na wanaomiliki silaha nchini humo.

 Msemaji wa jeshi ametangaza kukamatwa kwa watu 499 kusini mwa mji tete wa Daraa ikiwa ni wiki moja baada ya maelfu ya wanajeshi waliokuwa na vifaru walipovamia mji huo na kuyavuruga maandamano. Kwa mujibu wa jeshi walinda usalama 2 wameuwawa pamoja na magaidi 10 huku wanajeshi wanane wakijeruhiwa na watu watano wakiwa na silaha wakakamatwa.

Hata hivyo upande mwingine tovuti ya upinzani inayoendesha harakati za mapinduzi ya Syria mwaka 2011 imesema kwamba vikosi vya usalama leo alfajiri viliingia katika eneo la mji wa Kafar Nubbol kilomita 320 kutoka mji mkuu Damascus na kuzivamia nyumba kadhaa ambapo waliwakamata watu 26. Tovuti hiyo imewatolea mwito Wasyria kote nchini kukusanyika kila siku mchana kuwaunga mkono wenzao katika mji wa Daraa na miji mingine iliyodhibitiwa na jeshi.

Syrien Präsident Bashar Assad 24.04.2011
Utawala wa rais Assad wakosolewa na Jumuiya ya KimataifaPicha: picture-alliance/dpa

Mamia ya wapinzani walikamatwa Jumapili wakiwemo kutoka mji wa Daraa na Douma mji ulioko nje kidogo ya Damascus baada ya watu kadhaa kuuwawa katika maandamano ya mwishoni mwa wiki. Makundi ya kutetea haki za binadamu yanasema kwamba idadi ya raia waliouwawa imeongezeka tangu kuzuka kwa maandamano dhidi ya utawala huo wa Syria mwezi Machi, mpaka sasa watu 580 wameuwawa.

Kutokana na hali ya mambo kuzidi kwenda kombo nchini Syria waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Alain Juppe hii leo ametoa tamko akisema kwamba utawala wa rais Bashar-al Assad utaanguka ikiwa utaendelea kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji. Waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron pia amelaani hatua ya serikali ya Syria kutumia nguvu nyingi dhidi ya waandamanaji na kuutolea mwito Ulimwengu kutoa shinikizo zaidi dhidi ya serikali hiyo, ingawa Uturuki kwa upande wake imeonya dhidi ya wanajeshi kutoka nje kuingilia mzozo wa  Syria. Marekani imeshazuia mali za kakake Assad, Maher anayeongoza jeshi lenye uwezo mkubwa la nchi hiyo, pamoja na maafisa wengine wa ngazi ya juu na shirika la ujasusi la Syria. Umoja wa Ulaya unaandaa vikwazo vikiwemo vya silaha dhidi ya taifa hilo.

Mwandishi Saumu Mwasimba

Mhariri Josephat Charo.