1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapinzani wa serikali ya Burundi wadai kuteswa

12 Januari 2016

Wapinzani wa serikali nchini Burundi wanatoa madai juu ya kuteswa na polisi, wanajeshi na maafisa wa idara za usalama. Pia Kanali mmoja anatuhumiwa kuhusika

https://p.dw.com/p/1Hbnu
Wanajeshi wa Burundi katika mitaa ya mji mkuu Bujumbura
Wanajeshi wa Burundi katika mitaa ya mji mkuu BujumburaPicha: picture-alliance/blickwinkel/Blinkcatcher

Mtu mmoja amedai kwamba polisi walimpiga na mkanda na pia walimpiga mateke, kati kati ya barabara , katika mji mkuu Bujumbrura. Mtu huyo ambae hakutaka kutajwa jina alikamatwa na watu wa idara ya usalama katika kitongoji cha Cibitoke, kinachohesabika kuwa mojawapo ya ngome kuu za wapinzani nchini Burundi.

Sababu ya kukamatwa ameeleza mtu huyo ni kushiriki katika maandamano ya kupinga muhula wa tatu wa Rais Pierre Nukurunziza.

Ameeleza kwamba baada ya kufikishwa kwenye kituo cha polisi cha Ndadaye mjini Bujumbura aliteswa. Mtu mwengine,mwanamke pia amearifu kwamba yeye na wenzake walipigwa fimbo na polisi kana kwamba polisi hao walikuwa wanaua nyoka. Amesema baadhi yao walipigwa vibaya zaidi.

Madai hayo ni mazito na thabiti, na yanaelekezwa kwa serikali ya Burundi.

Madai hayo yanaelekezwa kwa polisi, jeshi na idara za usalama za nchi hiyo.

Mnamo mwezi wa Agosti mwaka uliopita Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International tayari lilitoa malalamiko juu ya jinsi polisi na wanajeshi wanavyowatesa watu ili kuuvunja upinzani katika bara bara za nchini Burundi.

Katika mahojiano na DW, wahanga wameyataja hata majina na vyeo vya maafisa waliowatesa. Wamesema miongoni mwa watesaji alikuwamo Kanali anaefanya kazi kwenye wizara ya ulinzi.

Wajumbe wakutana kujaribu kuleta suluhisho nchini Burundi
Wajumbe wakutana kujaribu kuleta suluhisho nchini BurundiPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Wandera

Kanali huyo anawakamata watu kutokana na madai kwamba wanashiriki katika maandamano.Waliokamatwa na Kanali huyo wamedai kwamba, aliwapeleka nyumbani kwake na kuwatesa, wakati mwingine kwa muda wa siku nzima. Lakini wakati mmoja , watu watatu walifanikiwa kukimbia.Hata hivyo Kanali huyo alikimibizana na watu hao na kumpiga risasi mmoja.

Msemaji wa serikali akanusha madai

Juu ya madai hayo, kaimu msemaji wa Rais Pierre Nkurunza amejibu kwa kusema kwamba hajasikia lolote juu ya madai hayo. Msemaji huyo Jean -Claude Karerwa Ndenzako ameeleza kuwa serikali ya Burundi inafanya bidii kuwasaka wahalifu ili waadhibiwe. Msemaji huyo pia amedai kwamba siyo wote waovaa sare ni polisi wa kweli.

Amedai kwamba zipo sare bandia za polisi zilizopo mitaani.Amesema panahitajika muda na subira katika kuyashuhgulikia madai yanayotolewa.

Mjumbe wa kanisa la Ujerumani, anaeratibisha misaada katika Afrika ya kati, Gesine Ames amesema uchunguzi uliofanywa na serikali ya Burundi haujaleta matokeo yoyote mpaka sasa, na wala hakuna wajumbe huru wa kufanya uchunguzi huo.

Mwandishi: Friederike Müller Jung.

Mfasiri:Mtullya Abdu.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman