1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapinzani waitisha maandamano Syria

18 Novemba 2011

Waasi wa Syria wanáandamana leo kuwashinikiza viongozi wa dunia wawafukuze mabalozi wa Syria na wazidi kuitenga serikali ya Damascus huku Uturuki ikionya vita vya wenyewe kwa wenyewe visije vikaripu Syria.

https://p.dw.com/p/13Cs2
Waandamanaji wa Syria na Uturuki dhidi ya rais Bashar al AssadPicha: picture-alliance/dpa

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa, Alain Juppé ambaye nchi yake ilikuwa mshika bendera katika opereshini za jumuiya ya kujihami ya NATO nchini Libya, yuko Uturuki tangu jana kwa mazungumzo kuhusu Syria.Baada ya mazungumzo yake pamoja na spika wa bunge la Uturuki, mwanadiplomasia huyo wa Ufaransa amesema tunanukuu "Wakati wa Syria kuanzisha mageuzi umeshapita."Mwisho wa kumnukuu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa aliyekuwa na mazungumzo pia hapo awali na waziri mkuu wa Uturuki, Recep Tayyeb Erdogan, na waziri mwenzake, Ahmet Davutoglu.

Akizungumza na maripota wa shirika la habari la Ufaransa, AFP, Ahmet Davutoglu amezungumzia hofu za kuripuka vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.

"Katika wakati ambapo wanajeshi wameshaanza kuasi na kupigana na jeshi la serikali, ninahisi kuna hatari ya mapigano hayo kuchukua sura ya vita vya wenyewe kwa wenyewe" amesema hayo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki.

Flash-Galerie Arabischer Frühling Jahresrückblick Syrien
Kiti kitupu cha Syria katika mkutano wa mawaziri wa jumuia ya nchi za kiarabu mjini Rabat-MorokoPicha: dapd

Jana vikosi vya serikali viliwauwa watu wasiopungua wanane, wakiwemo watoto wawili, licha ya onyo la jumuia ya nchi za kiarabu kwa Syria kuitaka ikomeshe matumizi ya nguvu la sivyo itawekewa vikwazo.

Wanaharakati wameitisha maandamano mengine hii leo na kuyatolea mwito mataifa yote ya dunia na yale ya kiarabu yawafukuze mabalozi wa Syria.

Wakati huo huo, Marekani haikubaliani na hoja za Urusi inayosema mashambulio ya wanajeshi walioasi yanaweza kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Urusi inapinga juhudi za nchi za magharibi za kuupa sura ya kimataifa mgogoro wa Syria, ikihofia jambo hilo lisije likazifungulia njia nchi za magharibi kuingia kijeshi nchini Syria kama ilivyotokea nchini Libya.

Mjini New York, mataifa ya magharibi yamesema jana yamejipatia uungaji mkono wa mataifa muhimu ya kiarabu kwa mswaada wa azimio la umoja wa mataifa linalolaani jinsi utawala wa Syria unavyovunja haki za binaadamu.

"Ulimwengu wa kiarabu umetoa mwito bayana, visa vinavyokwenda kinyume na haki za binaadam lazima vikome," amesema balozi wa Ujerumani katika Umoja wa mataifa, Peter Wittig.

Treffen EU-Außenministerrat Brüssel Catherine Ashton
Muakilishi mkuu wa siasa ya nje ya Umoja wa ulaya bibi Catherine AshtonPicha: dapd

Wakatai huo huo, muakilishi mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, bibi Catherine Ashton, amemualika mkuu wa jumuiya ya nchi za kiarabu,Nabil al Arabi, ashiriki katika mkutano wa umoja wa Ulaya Desemba mosi ijayo ili kuandaa kwa pamoja mikakati ya kuzidi kuishinikiza serikali ya Damascus.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/AFPE

Mhariri:Josephat Charo