1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapinzani wanne DRC wataka uchaguzi ubatilishwe

Admin.WagnerD30 Novemba 2011

Wagombea wanne waliosimama dhidi ya Joseph Kabila kugombea urais katika uchaguzi wa Jumatatu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanaomba uchaguzi huo ubatilishwe.

https://p.dw.com/p/13JUz
Waangalizi wanasema upigaji kura ulikumbwa na visa vya udanganyifu
Waangalizi wanasema upigaji kura ulikumbwa na visa vya udanganyifuPicha: picture-alliance/dpa

Hatua ya wagombea hao wa upinzani imefuatia ripoti za waangalizi kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na visa vingi vya udanganyifu. Ripoti za waangalizi wa uchaguzi wa tarehe 28 Novemba nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zinaonyesha kuwa zoezi la upigaji kura lilighubikwa na visa vingi vya ulaghai, vikiwemo kuongeza makaratasi ya kura katika masanduku, makaratasi ya kupigia kura ambayo hayakufikishwa kwenye vituo vilivyokusudiwa, na watu wengi waliokatazwa kupiga kura zao.

Wagombea hao wanaushutumu upande wa Rais Joseph Kabila kusababisha matatizo mengi kwenye vituo vya kupigia kura, wakisema wakala wao walikatazwa kuingia kwenye vituo vya kupigia kura, na kwamba baadhi ya vituo havikufunguliwa kabisa.

Kengo wa Dondo, mmoja wa wagombea wanaotaka kubatilishwa kwa uchaguzi.
Kengo wa Dondo, mmoja wa wagombea wanaotaka kubatilishwa kwa uchaguzi.Picha: AP

Jean Claude Katende kutoka shirika la kutetea haki za binadamu la ASADHO mjini Kinshasa amesema visa vilivyotokea ni vingi kiasi kwamba haviwezi kupuuzwa.

''Tunasema kwamba kulikuwa na matatizo kwa sababu hata tume ya uchaguzi yenyewe imekiri kuwa hata watoto walipiga kura. Mbali na watoto hao, tume hiyo pia inasema kuna watu 19 elfu ambao walipiga kura zaidi ya mara moja. Visa vyote hivyo vinathibitisha wasi wasi wa asasi za kiraia na wa upinzani. Hata mienendo ya polisi haikuwa watu nafasi ya kupiga kura yao kwa uhuru.'' Alisema Katende.

Mtu anayechukuliwa kuwa mpinzani mkuu wa Rais Joseph Kabila katika uchaguzi huu, Etienne Tshisekedi, hakujiunga na wagombea hawa wanne kutaka uchaguzi huu ubatilishwe. Mameneja wa kampeni yake walisema bado wanakusanya taarifa kutoka sehemu zote za nchi.

Lakini mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Daniel Ngoy Mulunda, anasema hakuna sababu yoyote ya kubatilisha uchaguzi. Bwana Mulunda anasema asilimia tisini na tisa ya vituo vya kupigia kura vilifunguliwa siku ya kwanza ya uchaguzi, na kwamba matatizo yaliripotiwa katika vituo 485 tu kati ya vituo 64 elfu.

Wapinzani wanadai Polisi haikuwasaidia watu kupiga kura kwa uhuru
Wapinzani wanadai Polisi haikuwasaidia watu kupiga kura kwa uhuruPicha: PA/dpa

Matokeo kamili ya uchaguzi wa rais yanasubiriwa tarehe sita mwezi ujao wa Desemba, na yale ya uchaguzi wa wabunge wiki moja baadaye. Mmoja wa waangalizi wa kutoka nchini Kongo aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba ana wasi wasi huenda kipindi hiki cha kusubiri kikawa cha mivutano mingi.

Wakati hayo yakiripotiwa, baraza la usalama la umoja wa mataifa limemwekea vikwazo Ntabo Ntaberi Shaka, kamanda wa wanamgambo wa Mai Mai mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kwa shutuma za kusimamia vitendo vya ubakaji dhidi ya mamia ya wanawake.

Katika tangazo la pamoja, Marekani, Uingereza na Ufaransa zimeiomba serikali ya Kinshasa kumkamata kamanda huyo ambaye licha ya kuwepo kwa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwake, aliruhusiwa kugombea ubunge katika uchaguzi huu uliomalizika.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/AFP

Mhariri:Miraji Othman