1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Warohingya: Umoja wa Mataifa watoa onyo

Zainab Aziz
24 Novemba 2017

Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema hali katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar sio salama kuwarejesha wakimbizi wa Rohingya ambao wamekimbilia Bangladesh kwa.

https://p.dw.com/p/2oD6I
Bangladesch | Rohingya-Flüchtlingslager rund um Cox's Bazar
Picha: DW/ P. Vishwanathan

UNHCR imesema ingawa bado halijayaona makubaliano ya kurejeshwa wakimbizi hao wa Rohingya yaliyotiwa saini jana Alhamisi, lakini linasisitiza kwamba kurudishwa kwa wakimbizi hao ni lazima kuzingatie hali ya usalama wao na pia warudishwe kwa hiari yao bila ya kulazimishwa. Msemaji wa shirika hilo, Adrian Edwards amewambia waandishi wa habari kwamba viwango vya kimataifa vizingatiwe na kwamba wao wako tayari kusaidia:

Wakimbnizi
Wakimbizi katika eneo linalosimamiwa na UNHCRPicha: DW/S. Tanha

Msemaji huyo wa UNHCR amesema kwa sasa hali katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar haifai na wala sio salama kuwarudisha wakimbizi. Mpaka sasa bado watu wanaendelea kukimbia na wengi wao wamekubwa na mateso, wengine wamebakwa na pia wana matatizo ya kaiakili. Wengine wao wameshuhudia mauaji ya jamii zao na marafiki. Wengi wao hawaoni hata sababu ya kurejea mahala ambako kila kitu chao kimeharibiwa. Pia kuna mgawanyiko mkubwa baina ya jamii ambao bado haujatafutiwa ufumbuzi. Edwards amesema bado ni shida kubwa hata kulifikia jimbo la kaskazini la Rakhine.

Vikundi vya watetezi wa haki za binadamu vimetoa wito kwamba mashirika ya kimataifa yaruhusiwe kufuatilia zoezi hilo la kurejeshwa kwa maelfu ya jamii ya Waislamu wa Rohingya kutoka Bangladesh kwenda nyumbani  Myanmar ambako walikukimbia miezi mitatu iliyopita, kufuatia hatua jeshi kuvamia vijiji na kuyachoma makaazi yao kwa madai ya kupambana na vikosi vya kigaidi.

Kwa mujibu wa makubaliano ya jana kati ya serikali hizo mbili za Myanmar na Bangladesh, kumekubaliwa mchakato utakaotumiwa katika zoezi hilo linalotarajiwa kuanza katika kipindi cha miezi miwili ijayo, lengo hasa likiwa ni kupunguza shinikizo katika kambi za wakimbizi ambazo zimeongezeka katika eneo la Cox Bazar nchini Bangladesh.

Kiongozi wa Myanmar - Aung San Suu Kyi
Kiongozi wa Myanmar Aung San Suu Kyi Picha: Reuters/E. Su

Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya zinaelezea hatua zilizochukuliwa na jeshi la Myanmar kama ni mauaji ya kikabila. Kiongozi wa kiraia wa Myanmar, Aung San Suu Kyi, amesema kurudi nyumbani kwa jamii ya Waislamu wachache kutakuwa kwa hiari. Kulikuwepo na wasiwasi kwamba jeshi la nchi hiyo linaweza kuleta pingamizi.

Mwandishi: Zainab Aziz/RTRE/DPAE

Mhariri: Mohammed Khelef