1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasenge washambuliwa Moscow

Thelma Mwadzaya28 Mei 2007

Polisi nchini Urusi wamewakamata wanaharakati wa kimataifa wanaotetea haki za wasenge katika maandamano mjini Moscow.Maandamano hayo yalikuwa yakifanyika nje ya ofisi ya meya hapo jana.

https://p.dw.com/p/CHkm
Wanaharakati wa haki za wasenge wakiandamana mjini Moscow
Wanaharakati wa haki za wasenge wakiandamana mjini MoscowPicha: picture alliance/ dpa

Wanaharakati hao walishambuliwa pia na wafuasi wa kanisa la Orthodox walio na msimamo mkali.Kiongozi wa jamii ya wasenge nchini humo Nikolai Alexeyev na wanaharakati wengine walikamatwa na polisi wakati maandamano hayo yakianza.

Raia walio na msimamo mkali wa Urusi waliwashambulia waandamanaji hao kwa kuwarushia mayai na kuwapiga kumbo kabla polisi wa kupambana na ghasia kuingilia kati ili kuwatawanya.

Baadhi ya waliokamatwa ni mwanaharakati wa zamani wa Uingereza Peter Tatchell,Marco Cappato mbunge wa Bunge la Ulaya kutoka Italia vilevile Volker Beck mbunge wa hapa Ujerumani.

Suala si kama Warusi wengi wanapenda amisah ya usenge na usagaji.Suala lililopo hapa ni je dola inawalinda walio wachache? Hilo ndilo jukumu ambalo Urusi kutokana na mikataba iliyotia inatakiwa ibebe na pale inaposema inataka kuwa jamii ya kidemokrasia.

Bwana Cappato aliachiwa baada ya kuzuiliwa kwa saa nne hivi kulingana na ubalozi wa Italia nchini humo.

Wanaharakati hao walipigwa ngumi usoni huku waandishi wa habari na polisi wakitazama.Nikolai Alexeyev alikuwa akijaribu kuwasilisha waraka wa kuomba ruhusa ya kufanya maandamano hayo katikati ya mji wa Moscow.

Barua hiyo ilitiwa saini na zaidi ya wabunge 40 wa Bunge la Umoja wa Ulaya.Meya wa mji Yury Luzhkov amekuwa akikataa kila wakati kuruhusu maandamano ya aina hiyo kufanyika.Kiongozi huyo alielezea mkutano huo kuwa vitendo vya kishetani.

Bwana Beck alipigwa mwaka jana pia katika maandamano ya kwanza ya wasenge yaliyofanyika mjini Moscow.

Wabunge kutoka nchi za Italia,Ujerumani na Austria wanaunga mkono maandamano hayo likiwemo pia kundi maarufu la muziki la Urusi kwa jina Tatu.Kulingana na Yuliya Katina muimbaji wa kundi hilo hakuna anayepaswa kuamuru namna ya kumpenda mtu yeyote yule.

Wasenge nchini Urusi hawachukuliwi vizuri tofauti na Ulaya ya magharibi jambo linalowafanya kuendelea na shughuli zao kimya kimya.

Kabla maandamano hayo kufanyika msemaji wa polisi Viktor Biryukov aliwalaumu wanaharakati hao kwa kuzusha ghasia.Zaidi ya watu 100 walikamatwa mjini Moscow mwaka jana katika maandamano kama hayo yaliyopigwa marufuku.

Kukamatwa kwa wanaharakati hao wasenge kulizua kashfa kote barani Ulaya.Meya wa mji wa Roma vilevile mawaziri na wabunge wa Italia walipinga ghasia hizo.Shirikisho la Urusi na hasa mji wa Moscow halitimizi wajibi wao kwahivyo serikali ya Ujerumani inayoshikilia urais wa Jumuiya ya Ulaya haitakiwi kunyamaa kimya.

Baadhi ya viongozi katika Bunge la Umoja wa Ulaya walikubaliana kuwa suala hilo litajadiliwa mwezi ujao katika kikao cha G8 ili kutathmini iwapo Urusi inatimiza maadili ya Baraza la Ulaya ambayo ni mwanachama. Kwa mujibu wa Kituo cha wasenge,wasagaji na huntha kilichoko mjini Paris,Ufaransa waandamanaji waliokamatwa wanapaswa kuachiwa kwani wana wasiwasi huenda wakahukumiwa kifungo.