1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mustakabali wa Ujerumani waamuliwa

20 Julai 2015

Miaka 70 iliyopita viongozi wa madola yaliyoshinda vita vikuu vya pili walikutana katika mji wa Potsdam mashariki mwa Ujerumani kuujadili mustakabali wa Ujerumani. Jee viongozi hao waliyapitisha maamuzi gani?

https://p.dw.com/p/1G0PS
Berlin Potsdamer Platz 1946
Picha: picture-alliance/akg-images

Baada ya Ujerumani kusalimu amri tarehe 8 mwezi Mei mnamo mwaka wa 1945, viongozi wa madola yaliyoshinda vita,kutoka Marekani,Urusi na Uingereza walikutana katika mji Potsdam ili kujenga mfumo mpya wa utawala nchini Ujerumani.

Rais wa Marekani, Harry Truman,Waziri Mkuu wa Uingereza,Winston Churchil na Kiongozi wa Urusi Joseph Stalin walikusudia kuweka mfumo mpya wa amani kutokea Ujerumani. Viongozi hao wa nchi zilioshinda vita, walikusudia kuziweka taratibu za malipo ya fidia pamoja na misingi ya kisiasa na kiuchumi. Lakini awali ya yote yalikuwapo masuala ya msingi juu ya jinsi ya kuhusiana na Ujerumani.

Akihutubia kwa njia ya Radio Rais wa Marekani wa wakati huo Harry Truman alisema ,kwenye mkutano wao mjini Potsdam viongozi wa madola yaliyoshinda vita walikubaliana juu ya kuifagilia mbali itikadi ya kifashisti na kuiteketeza sekta yote ya kijeshi. Lengo lilikuwa kuondoa kila kitu ambacho kingeliweza kutumiwa kwa ajili ya kufanyia matayarisho ya vita vingine.

Mauerfall-Projekt: Potsdam, 1987/88
Picha: Robert-Havemann-Gesellschaft

Mazungumzo ya madola makuu matatu kama yalivyokuwa yanaitwa wakati huo, yalianza majira ya saa 11 jioni katika mji wa Potsdam. Meza ya mazungumzo ililetwa kutoka Urusi.Lakini mazungumzo yalikwama tokea mwanzoni.Waziri Mkuu wa Uingereza, wa wakati huo Winston Churchill alitaka ufafanuzi juu ya Ujerumani.

Hayakuwa tu maslahi ya washindi wa vita kuiweka Ujerumani, haraka chini ya udhibiti wao bali pia ilihusu maeneo yaliyopaswa kudhibitwa na kila nchi iliyoshinda vita na hivyo kuyapa kipaumbele maslahi yake barani Ulaya.Hatimaye madola yaliyoshinda vita yalikubaliana na pendekezo la Rais Harry Truman juu ya kuigawanya Ujerumani kati ya mashariki na magharibi.

Pamoja na hayo washindi wa vita walikubaliana juu ya kutoa mamlaka kamili kwa kila sehemu iliyokaliwa na washindi. Ufaransa iliingizwa baadae kuwa miongoni mwa wasimamizi wa Ujerumani. Kwa kifupi Ujerumani ilikuwa imepoteza umoja wake wa kijografia,kiuchumi na kisiasa. Lakini maeneo hayo yaliyokaliwa ndiyo yaliounda Jamhuri ya kidemokrasai ya Ujerumani na Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani. Lakini maamuzi hayo ndiyo baadae yaliyosababisha mvutano baina ya nchi za magharibi na Umoja wa Kisoviet- ndiyo ulikuwa mwanzo wa vita baridi baina ya magharibi na mashariki.

Mazungumzo ya viongozi wa nchi zilizoshinda vita vikuu vya pili yaliendelea hadi mwezi wa Agosti kabla ya kutolewa tamko la Potsdam.Mpaka wa Poland ulibadilishwa na Poland ilipaswa kulipwa fidia na iliingizwa katika himaya ya kisoviet. Viongozi hao pia walikubaliana juu ya fidia ambayo Ujerumani ilipaswa kulipa. Na kila upande ulilipa kwa mujibu wa makubaliano na washindi wa vita.Hata hivyo mkutano wa mjini Potsdam ulitoa ishara ya matumaini kwa Wajerumani. Mlango ulikuwa wazi kwa Ujerumani kurejea katika jumuiya ya kimataifa.

Mwandishi: Bosen, Ralf.
Mfasiri:Mtullya abdu