1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON: Baraza la usalama kuijadili Iran wiki ijayo

23 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCPN

Naibu waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Nicholas Burns, amesema wanachama watano wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani wataujadili mpango wa nyuklia wa Iran mjini London Uingereza Jumatatu wiki ijayo.

Burns aliwaambia waandishi wa habari mjini Washington kwamba Marekani itataka azimio jipya la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa litayarishwe ili kuitenga Iran kwa kushindwa kutimiza agizo la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa la kusitisha shughuli zake za kurutubisha uranium kwa wakati uliowekwa.

Nicholas Burns alikuwa akizungumza saa chache baada ya shirika la kimataifa la kuzuia usambazaji wa silaha za kinyuklia, IAEA, kuwasilisha ripoti yake iliyosema kwamba Iran imepuuza tarehe ya mwisho ya kusitisha urutubishaji wake wa uranium. Aidha ripoti hiyo iliishtaki Iran kwa kuongeza shuhguli zake katika mpango wake wa nyuklia.

Msemaji wa wizara ya mashauri ya kigeni nchini Marekani, Tom Casey, amesema jumuiya kimataifa bila shaka itaichukulia hatua Iran kwa kukaidi agizo la baraza la usalama.

´Hakuna agizo lolote lililotimizwa. Azimio linasema baraza la usalama litakutana na kujadili hatua nyengine kufuatia hatua ya Iran kukataa kutii. Bila shaka tutafanya hivyo. Sitaki kusema lolote kwa sasa lakini kama waziri wa mambo ya kigeni alivyosema kuhusu kuunda azimio jipya, bila shaka kutakuwa na hatua zaidi zitakazochukuliwa na jumuiya ya kimataifa kufuatia Iran kukataa kutii.´

Baraza la usalama linahofu kwamba Iran huenda inataka kutengeza silaha za kinyuklia, lakini serikali ya mjini Tehran inasisitiza mpango wake wa nyuklia ni wa matumizi ya amani pekee.