1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON : Bunge lalani nia ya Bush kuongeza vikosi Iraq

17 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCRQ

Baraza la Wawakilishi la bunge la Marekani limepitisha azimio lenye kulaani azma ya Rais George W. Bush kuongeza wanajeshi zaidi nchini Iraq.

Azimio hilo ambalo halishurutishi limepita kwa kura 246 dhidi ya 182.Wabunge kumi na saba wa chama chake mwenyewe Bush cha Republican wameungana na wabunge wa chama cha Demokratik walio wengi bungeni kuunga mkono azimio hilo.Ikulu ya Marekani imelitupilia mbali karipio hilo kwa kusema kwamba Bush hafungiki kisheria na azimio hilo na kwamba hivi karibuni ataliomba bunge la Marekani kugharimia kikamilifu vikosi vya Marekani vilioko nchini Iraq.

Bush anapanga kupeleka wanajeshi 21,000 wa ziada nchini Iraq.Kura hiyo bungeni ni hatua ya kwanza ya kisheria kupinga jinsi Bush anavyoshughulikia vita vya miaka minne nchini Iraq ambavyo bunge iliidhinisha hapo mwezi wa Oktoba mwaka 2004.

Tokea uvamizi ulioongozwa na Marekani nchini Iraq hapo mwaka 2003 wanajeshi wa Marekani 3,100 na maelfu kwa maelfu ya wananchi wa Iraq wameuwawa.