1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Washington: Bush afikiria kuongeza wanajeshi Irak

20 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CChj

Ikulu ya Marekani imedhibitisha kwamba Rais George W. Bush anazingatia kuongeza kwa kipindi kifupi idadi ya wanajeshi wa Marekani nchini Iraq. Hivi sasa Marekani ina wanajeshi kiasi ya 140,000 nchini humo . Katika mahojiano na gazeti moja, Rais Bush alisema anapanga kuongeza idadi ya wanajeshi kukabiliana na vita vipana zaidi na vya muda mrefu dhidi ya Ugaidi. Waziri mpya wa ulinzi Robert Gates ameombwa kuizingatia fikra hiyo. Mnamo siku ya Jumatatu, ripoti ya Wizara ya ulinzi ya Marekani –Pentagon- ilisema umwagaji damu nchini Irak umefikia kiwango kikubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu nchi hiyo ilipokabidhiwa mamlaka ya utawala 2004. Imesema idadi ya hujuma dhidi ya majeshi ya Marekani na Irak pamoja na raia imeongezeka kufikia 1,000 kwa wiki, huku maeneo ambako hali ni mbaya zaidi yakiwa ni mji mkuu Baghdad na mkoa wa magharibi wa Anbar, ambako kwa muda mrefu ni eneo la harakati za wapiganaji wa Kisunni.