1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON : Bush aionya Iraq dhidi ya Iran

10 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBaZ

Rais George W. Bush wa Marekani hapo jana amesisitiza kwamba Iran imekuwa ikidhoofisha Iraq licha ya madai ya Iran kwa Waziri Mkuu wa Iraq Nuri al- Maliki kwamba nchi hiyo imekuwa ikisaidia kuleta utulivu nchini humo.

Akiita Iran kuwa ni taifa la uchokozi sana ambalo lazima litengwe Bush ameonya wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika Ikulu ya Marekani kwa kusema kwamba ujumbe wake ni kwamba wakimfuma anatimiza dhima ya uharibifu nchini Iraq kutakuwa na gharama ya kulipa.

Bush ametowa kauli hiyo wakati al Maliki akiwa ziarani nchini Iran ambapo ameahidiwa msaada kamili wa kurudisha usalama nchini Iraq. Hata hivyo serikali ya Iran imemuieleza al Maliki kwamba umwagaji damu nchini Iraq utakomeshwa kwa kuondolewa kwa majeshi ya Marekani tu.

Al –Maliki anakabiliwa na matatizo ya kisiasa yanayozidi kuwa makubwa nchini Iraq na shutuma za Marekani kwamba hachukuwi hatua za kutosha katika kuondowa utengano wa kimadhehebu.

Wakati huo huo Rais Bush amesema kazi ya kuifunga kambi ya magereza ya Marekani huko Guantanamo haitokuwa rahisi.

Amesema kwamba kwa upande mmoja baadhi ya mataifa wanakotokea wafungwa hayana haja sana ya kuwachukuwa wafungwa hao nyumbani.Pia amesema kuwahamishia kwenye magereza yalioko katika ardhi ya Marekani sio chaguo linalofaa.

Marekani inawashikilia wafungwa 355 katika kambi ya Guantanamo ambayo ilianzishwa kushughulikia wafungwa waliotekwa na Marekani baada ya mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani.