1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON : Bush apanguwa makamanda waandamizi Iraq

6 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCd3

Rais George W. Bush wa Marekani ameufanyia mabadiliko uongozi wake wa kijeshi kwa Iraq kabla ya kutangaza mabadiliko ya sera kwa vita vya Iraq wiki ijayo huku akikabiliwa na upinzani wa chama cha Demokrat dhidi ya kuongeza wanajeshi nchini Iraq.

Bush amemteuwa Admireli William Fallon kuchukuwa nafasi ya Generali John Abizaid kama mkuu wa Makao Makuu ya Kijeshi ya Marekani anayeshughulikia operesheni za kijeshi za Marekani nchini Iraq na Afghanistan.

Pia amemuondowa kwenye wadhifa wake kama kamanda mkuu wa Marekani nchini Iraq Generali George Casey ambaye alielezea mashaka yake juu ya kuongezwa kwa vikosi vya Marekani nchini Iraq.Nafasi yake imechukuliwa na Luteni Generali David Petraeus ambaye alikuwa kamanda mkuu wakati wa uvamizi wa Iraq hapo mwaka 2003.

Generali Casey anakuwa Mnadhimu Mkuu wa Majeshi ya Marekani.

Ikulu ya Marekani imekanusha dhana kwamba Bush anafanya mabadiliko hayo ya makamnda wake kwa sababu hamwelezi kile anachotaka kukisia yeye.

Mabadiliko mengine muhimu aliyotangaza Rais Bush ni kuteuliwa kwa Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani CIA John Negraponte kuwa naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani na Makamo Admireli Mstaafu Michael McConnell kuchukuwa nafasi yake.

Mabadiliko hayo inabidi yaidhinishwe na baraza la Senate la bunge la Marekani.