1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON : Bush na Blair wakiri Iraq inahitaji mwelekeo mpya

8 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CClb

Rais George W. Bush wa Marekan na mshirika wake mkubwa katika vita vya Iraq Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair wametowa maoni yao juu ya repoti ilioandaliwa na jopo la vigogo wa Marekani inayoeleza kwamba sera yao nchini Iraq imeshindwa na kunahitajika mwelekeo mpya.

Katika mkutano na waandishi wa habari katika Ikulu ya Marekani Bush amekiri kwamba hali ni mbaya lakini amesema kwamba anasubiri repoti nyengine mbili za ziada kutoka kwa Wizara ya Ulinzi na Wizara ya mambo ya nje.Bush amesema atakubali tu kuitikia wito wa jopo hilo wa kuzijumuisha Iran na Syria katika mazungumzo juu ya Iraq iwapo nchi hizo zitakubali kukomesha kuunga mkono wafuasi wa itikadi kali na kuisaidia serikali dhaifu ya Iraq.

Blair amesema repoti hiyo inapendekeza njia madhubuti ya kupiga hatua mbele na kwamba ni jambo linalowezekana kuutatua mzozo wa Mashariki ya Kati kwa ujumla wake kwa mwelekeo wa kushughulikia kwa wakati mmoja mzozo wa Israel na Wapalestina.

Viongozi wote wawili Bush na Blair wamekiri kwamba mwelekeo mpya unahitajika kwa Iraq na mengi yanatakiwa kufanywa kuisaidia serikali ya nchi hiyo.