1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON : Harakati kuleta utulivu Mashariki ya Kati

29 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCoR

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condololeezza Rice atajaribu kuupa nguvu usitishaji tete wa mapigano kati ya Israel na Wapalestina wiki hii wakati atakapokutana na washirika wake wa Kiarabu wenye msimamo wa wastani katika juhudi za dharura za kuleta utulivu nchini Iraq.

Rice anatarajiwa kukutana na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina hapo kesho kwenye mji wa Ukingo wa Magharibi wa Jericho huku kukiwa na dalili za kupamba moto kwa hatua za kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ya Palestina ambazo hivi sasa zinaelezewa kuwa zimekwama.

Baadae katika mji wa kitalii ulioko karibu wa Bahari ya Chumvi Rice atakutana na mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa sita ya Ghuba.

Wakati umwagaji damu ukizidi kupamba moto katika eneo la Mashariki ya Kati utawala wa Rais George W Bush wa Marekani uko chini ya shinikizo zito la kubadili kabisa mkakati wake nchini Iraq.

Bush na Rice leo na kesho wanatarajiwa kujadili hatua za kuchukuwa kukabiliana na mgogoro huo katika mji mkuu wa Jordan Amman na waziri Mkuu wa Iraq Nuri al Maliki pamoja na Mfalme Abadallah wa Jordan.