1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON : Jaji azuwiya kuhamishwa mfungwa wa Guantanamo

10 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7Gy

Jaji wa mahkama ya serikali ya Marekani amezuwiya kuhamishwa kwa mfungwa mmoja kutoka Guantanamo kupelekwa nchini Tunisia.

Mfungwa huyo Mohamed Abdul Rahman amedai kwamba atateswa iwapo atarudishwa nchini mwake.Rahman anakabiliwa na matatizo ya moyo na hakimu ametowa hukumu kwamba kuhamishwa kwake kutasababisha madhara makubwa yasioweza kurekebishwa.

Uamuzi huo unapongezwa na mashirika ya haki za binaadamu kuwa wa kihistoria kwa sababu ni kwa mara ya kwanza kabisa kwamba hakimu wa mahkama ya Marekani ameingilia kati moja kwa moja kwa niaba ya mfungwa wa Guantanamo.

Wakati huo huo Mahkama Kuu ya Marekani imekataa kusikiliza rufaa ya mtu wa Ujerumani ambaye alitekwa nyara na shirika la ujasusi la Marekani CIA hapo mwaka 2003.

Khaled el Masri amekuwa akitaka aombwe radhi na kulipwa fidia ya takrtiban dola 75,000.Serikali ya Marekani imeitaka mahkama hiyo iikatae kesi hiyo kwa sababu za usalama wa taifa.

El Masri anadai alifungwa na kuteswa nchini Afghanistan kwa miezi kadhaa kabla ya kuachiliwa bila ya kupatiwa maelezo yoyote yale.Mahkama ya Ujerumani imetowa hati za kukamatwa kwa mashushu 13 wa Marekani inaoaminika kuhusika na kutekwa kwake nyara.

Kesi hiyo imeweka nadhari ya kimataifa kwa mpango tata wa CIA wa kurudishiwa watuhumiwa ambapo huwateka nyara watuhumiwa wa ugaidi na kuwahamisha kutoka nchi moja kwenda nyengine kwa ajili ya kuwasaili.