1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON: Kifungo cha maisha kwa mauaji ya 1964

25 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBWA

Nchini Marekani,mwanachama wa zamani wa kundi la ubaguzi wa rangi-Ku Klux Klan,amepewa adhabu ya kufungwa jela maisha kwa kuhusika na mauaji ya vijana wawili weusi katika jimbo la Mississippi katika mwaka 1964.

Askaripolisi wa zamani,James Ford Seale alie na miaka 72 ameadhibiwa vifungo vitatu vya maisha kwa hatia ya kutekanyara na kupanga njama kuhusika na mauaji ya Charles Eddie Moore na Henry Hezekieh Dee.Vijana hao wawili walikuwa na miaka 19 walipouawa.

Kesi hiyo ilifunguliwa tena mwaka 2005 baada ya kaka wa Moore kupigania kwa miaka na miaka kuwa kesi hiyo isikilizwe upya.Seale alikamatwa mara ya kwanza mwaka 1964,lakini aliachiliwa huru na polisi iliyosema kuwa haukuwepo ushahidi wa kutosha dhidi yake.

Kesi nyingi zinazohusika na mauaji ya ubaguzi wa rangi katika miaka ya 60,zimefunguliwa upya katika miaka ya hivi karibuni.