1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON: Marekani kuifutia deni Liberia

14 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCSD

Marekani imeahidi kuifutia Liberia deni la dola milioni 391. Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Bi Condoleezza Rice, alitoa tangazo hilo kwenye mkutano wa wahisani kuhusu Liberia mjini Washington Marekani.

´Marekani inaidai Liberia deni la dola milioni 391 ambalo mpaka sasa halijalipwa. Tutalifuta deni hilo! Lote! Katika mpango wa kuyasamehe mataifa yenye madeni makubwa.´

Vita vya miaka minne nchini Liberia vilisababisha vifo vya watu takriban laki mbili na kuiharibu miundombinu ya nchi hiyo. Akizungumza kwenye mkutano wa mjini Washington, rais wa Liberia,Ellen Johnson Sirleaf, ameonya kwamba hatari ya kurejea vitani miongoni mwa jamii zilizotoka vitani ni kubwa kama serikali na jumuiya ya kimataifa haiwezi kuchukua hatua madhubuti kwa wakati muhimu.

´Liberia leo iko katika mojawapo ya nyakati hizo muhimu. Hatujaondokana na matatizo yetu lakini juhudi zetu za pamoja katika miezi michache ijayo, mwaka ujao na kuendelea, zitaamua hali ya baadaye ya taifa.´

Condoleezza Rice amezitaka nchi za magharibi ziyasaidie mataifa ya Afrika magharibi. Waziri Rice pia amesema rais George W Bush amelitaka bunge la Congress liidhinishe dola milioni 200 kama msaada zaidi kwa Liberia kwa mwaka huu na mwaka ujao.