1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON : Mkakati wa Iraq kukabili wakati mgumu

25 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CByb

Rais George W. Bush wa Marekani amesema kwamba miezi michache ijayo itakuwa ya wakati mgumu kwa mkakati wa mpya wa Marekani kwa Iraq.

Akihutubia waandishi wa habari katika Ikulu ya Marekani Bush amesema kwamba anatarajia kuzuka kwa mapigano makubwa baada ya kuongezwa kwa wanajeshi wa Marekani nchini Iraq ifikapo kati kati ya mwezi wa Juni.

Kauli yake hiyo inakuja wakati bunge la Marekani likipiga kura kwa muswada wa kugharamia vita nchini Iraq na Afghanistan wa dola bilioni 120.Baraza la Wawakilishi limeidhinisha muswada huo kwa kura 280 dhidi ya 142 kugharamia vita vya Iraq hadi mwezi wa Septemba mwaka huu baada ya wabunge wa Demokrat kukubali shingo upande madai ya Bush ya kuondolewa kwa vipengele vinavyotaja tarehe ya kuondolewa kwa wanajeshi wa Marekani nchini humo.

Baraza la Senate nalo limeudhinisha muswada huo kwa kura 80 dhidi ya 14.

Rais Bush amesema Marekani lazima iwapatie wanajeshi wake fedha na rasilmali wanazohitaji kumshindwa adui nchini Iraq.

Mapema nchini Iraq mripuko wa bomu lililotegwa kwenye gari umeuwa takriban watu 30 na kujeruhi madarzeni wengine katika mji wa magharibi wa Falujjah.