1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON : Mtuhumiwa apunguziwa kifungo

31 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCDv

David Hicks mfungwa wa Australia anaeshikiliwa katika kambi ya kijeshi ya Marekani katika gereza la Guantanamo nchini Cuba amesaini makubaliano ya kukubali kukiri ambayo yanapunguza adhabu yake ya kuunga mkono ugaidi kuwa kifungo cha miaka saba gerezani.

Chini ya makubaliano hayo kati ya serikali ya Marekani na Australia Hicks mwenye umri wa miaka 31 atatumikia kifungo chake nchini Australia.Hapo Jumatatu alikiri kuwa na hatia kwa madai ya kutowa msaada wa vifaa kwa ugaidi.

Hicks alikamatwa kama mtuhumiwa wa ugaidi na majeshi ya muungano yaliokuwa yakiungwa mkono na Marekani hapo mwaka 2001 nchini Afghanistan.

Wakati huo huo mtuhumiwa wa ugaidi wa Saudi Arabia ameliambia baraza la mahkama la kijeshi la Marekani kwamba aliteswa kumfanya akiri kwamba alikuwa amehusika katika uripuaji wa meli ya kivita ya Marekani.

Abdulrahim al Nashiri amesema imebidi atunge uongo kumhusisha na shambulio la Meli ya Marekani ya USS Cole ili kukomesha kuteswa.Wanamaji 17 wa Marekani walikufa katika shambulio hilo la mwaka 2002 wakati meli hiyo ya kivita ilipokuwa imeegesha bandarini nchini Yemen.

Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani amesema kwamba madai yoyote yale juu ya kuteswa yatafanyiwa uchunguzi.