1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON: Rais Bush ashinda mjadala kuhusu kulidhamini jeshi

23 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CBzH

Rais George W Bush wa Marekani, ameshinda mjadala mkali kuhusu utoaji wa fedha kwa ajili ya vita nchini Irak na Afghanistan.

Wakikabiliwa na kura ya turufu, viongozi wa chama cha Democratic katika bunge la Marekani wanakaribia kukubaliana na utawala wa rais Bush kuhusu mswada wa kutoa fedha zaidi kwa ajili ya vita nchini Irak na Afghanistan.

Makubaliano hayo hata hivyo hayaweki tarehe ya kuondoka wanajeshi wa Marekani kutoka uwanja wa vita.

Maafisa kadhaa wanasema mswada huo huenda ukagharimu kiasi cha dola bilioni 120, ikiwa ni pamoja na dola bilioni nane za chama cha Democratic kwa matumizi ya ndani ya nchi, kiwango kilichopingwa hapo awali na ikulu ya Marekani. Kiwango hicho kinajumulisha fedha za kuwasaidia wahanga wa kimbunga Katrina na wakulima wa Marekani walioathiriwa na ukame.

Wabunge wa chama cha Republican na Democratic wana matumaini makubaliano yatakayofikwa baina ya vyama hivyo yatawasilishwa kwa rais Bush kesho kutwa Ijumaa ili atie saini.