1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON : Rais Bush haridhishwi na hali ya Iraq

5 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCmR

Rais George W. Bush wa Marekani ameelezea kutoridhishwa kwake na hali nchini Iraq.

Akizungumza na Abdel Aziz al Hakim mwanasiasa mashuhuri wa Kishia nchini Iraq katika Ikulu ya Marekani Bush amemweleza hakuridhishwa na kasi ya maendeleo nchini Iraq na baadae alikiambia kituo cha televisheni cha Fox News kwamba kile Wamarekani wanachojaribu kutafakari ni kwa nini Wairaqi wanawauwa Wairaqi wenzao wakati wakiwa na mustakbali mzuri mbele yao.Hata hivyo Bush amesema anathamini kazi ya al Hakim na Waziri Mkuu wa Iraq Nouri al Maliki kuiunganisha nchi hiyo.

Baada ya mazungumzo yake na Bush kiongozi huyo wa Baraza Kuu la Mapinduizi ya Kiislam nchini Iraq linaloungwa mkono na Iran al Hakim amesema njia pekee ya kuepusha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Iraq ni kwa majeshi ya Marekani kushambulia kwa nguvu kubwa zaidi waasi wanaongozwa na Wasunni.

Awali al Hakim alikutana na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleezza Rice katika kile alichoeleza kuwa yalikuwa mazungumzo ya wazi na kusema kwamba Iraq inapaswa kuwa katika nafasi ya kujiamulia mambo yake yenyewe.

Hapo jana wanajeshi wanne wa Marekani waliuwawa wakati helikopta yao ilipoanguka kwenye jimbo tete la Al-Anbar.