1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON: Rice asema Marekani haitaivamia Korea Kaskazini

11 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD3u

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Bi Condoleezza Rice, amesema Marekani haitaivamia Korea Kaskazini kufuatia jaribio lake la kinyuklia. Aidha Rice amekanusha madai kwamba Korea Kaskazini inataka iwe na silaha za kinyuklia ili kuzuia uvamizi wa Marekani kama ule wa Irak.

Condoleezza Rice amesema ipo haja ya kurudi kwenye mazungumzo ya mataifa sita.

´Korea Kaskazini ilianza mpango wake wa silaha za nyuklia miongo kadhaa iliyopita na ukweli ni kwamba jumuiya ya kimataifa hatimaye inatakiwa kuungana katika hali itakayoileta China, Korea ya Kusini na washikadau wote kwenye meza ya mazungumzo. Ikiwa tutafikia makubaliano na Korea Kaskazini kuharibu mifumo yake ya silaha za kinyulklia, makubaliano hayo yaweze kweli kuwa na nafasi ya kudumu.´

Jana waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe alitoa mwito serikali ya Pyongyang iwekewe vikwazo vitakavyoiumiza. Rais wa Korea Kusini, Roh Moo-Hyun kwa upande wake aliitaka jumuiya ya kimataifa iyajadili maoni ya Korea Kaskazini kabla kuiadhibu.