1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON : Wiki ya kidiplomasia kwa Mashariki ya Kati

27 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCoq

Rais George W. Bush wa Marekani akiwa chini ya shinikizo la kutafuta suluhisho la Iraq ameondoka kuelekea Riga nchini Latvia kwa ajili ya mkutano wa viongozi wa Umoja wa Kujihami wa Mataifa ya Magharibi NATO ambapo anataraji kuwashinikiza washirika wake wa Ulaya kutowa msaada zaidi kwa Afghanistan.

Lakini suala kuu katika mkutano huo wa siku mbili linaendelea kuwa mapambano nchini Iraq.Serikali ya Marekani imefadhaishwa kutokana na mojawapo ya wiki za umwagaji mkubwa wa damu kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka miatu tokea Marekani ivamie nchi hiyo.Hapo Alhamisi watu wanaokaribia 300 waliuwawa nchini kote Iraq.

Bush ataelekea nchini Jordan mara tu baada ya kumalizika kwa mkutano huo wa viongozi wa NATO mjini Riga na kuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu wa Iraq Nuri al Maliki.Mfalme Abdallah wa Jordan ambaye atakuwa mwenyeji wa mkutano ametahadharisha juu ya uwezekano wa kuzuka kwa vita vitatu vya wenyewe kwa wenyewe Mashariki ya Kati.

Mfalme huyo wa Jordan ameongeza kusema kwamba mizozo hiyo haiwezi kutenganishwa na kwamba lazima itatuliwe kwa ujumla wake.

.