1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON : Wolfowitz alijiamulia peke yake

13 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CCAL

Bodi ya wakurugenzi ya Benki ya Dunia imesisitiza kwamba rais wa benki hiyo Paul Wolfowitz katu hakuwahi kupata idhini ya ongezeko kubwa la mshahara ambayo wanasema aliamuru binafsi kulipwa mwanamke wake katika chombo hicho kinachotowa mikopo duniani.

Bodi hiyo imeahirisha mkutano hapo jana hadi leo hii juu ya mpango wa ajira wenye thamani ya karibu dola 200,000 ambao Benki ya Dunia ilimpa mwanamke huyo wa Wolfowitz.

Wolfowitz amekiri hapo jana na kuomba radhi kwamba alifanya makosa katika kulishughulikia suala la mwanamke wake huyo Shaha Riza ambaye alifanya kazi katika benki hiyo kwa miaka minane kama afisa mwandamizi wa mawasiliano kabla ya kupangiwa kazi katika wizara ya mambo ya nje.

Katika taarifa bodi ya wakurugenzi watendaji wa benki hiyo imesema imegunduwa kwamba sababu na masharti ya kupandishwa cheo na mshahara kwa Riza hayakupitiwa na kamati ya maadili ya benki hiyo wala mwenyekiti wa bodi kabla ya kuidhinishwa na Wolfowitz muda mfupi baada ya kujiunga na taasisi hiyo hapo mwaka 2005.

Wafanya kazi wa benki hiyo kuu ya dunia wanataka Wolfowitz ajiuzulu.