1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Washington.Condoleezza Rice azitaka nchi za Asia kuunga mkono vikwazo ilivyowekewa Korea ya Kaskazini.

17 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD1z

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Bibi Condoleezza rice amesema, anamatumaini kwamba Korea ya Kaskazini haitafanya jaribio la pili la bomu la nyuklia, baada ya maafisa upelelezi wa Marekani, kuthibitisha kwamba mripuko wa wiki iliyopita ulikuwa ni wa bomu la nyuklia.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Washington, Condoleezze Rice vile vile ameionya Iran kwamba vikwazo vya Umoja wa Mataifa ilivyoiwekea Korea ya Kaskazini, lazima viwe ni changamoto kwa harakati za Iran kuendelea na mpango wake wa nyuklia.

Bibi Rice alizitaka nchi zote barani Asia kuridhia vikwazo vilivyowekwa na Baraza la Usalama laUmoja wa Mataifa na kuchangia kikamilifu katika makubaliano hayo ili shinikizo hilo lionyeshe matokeo yake katika uchumi wa Korea ya Kaskazini.

Aidha aliendelea kwa kusema.

”Korea ya Kaskazini, haiwezi kuhatarisha ulimwengu, na kutaraji mataifa mengine yatafanya nayo biashara kama kawaida ya zana za kutengeneza silaha au makombora. Haiwezi kukorofisha mfumo wa kimataifa na kutaraji kutumia mitandao ya kifedha iliyoandaliwa kwa ajili ya biashara ya amani, Azimio nambari 1718 linaweka wazi. Tunataraji kila mwanachama wa Jumuiya ya kimataifa, atatekeleza kikamilifu, vipengee vyote vya azimio hilo na tunataraji baraza la usalama litachunguza kwa makini utekelezaji wake”.

Bibi Rice leo anatarajiwa kusafiriri kuelekea Japan, Korea ya Kusini na China ili kutafutwa kuungwa mkono kufuatiwa azimio la Umoja wa Mataifa la kuiwekea vikwazo Korea ya Kaskazini.