1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Washirika wa kisiasa wa Merkel wazidi kumtia kishindo

Admin.WagnerD8 Septemba 2016

Washirika wa kisiasa wa Kansela Angela Merkel - chama cha Christian Social Union CSU, wameongeza shinikizo kwake akaze sheria za uhamiaji na ukimbizi kwa kutaka kipaumbele wapewe wahamiaji Wakristo.

https://p.dw.com/p/1Jyb7
Bundeskanzlerin Angela Merkel
Picha: picture-alliance/dpa/D. Karmann

Chama hicho cha CSU pia kimetaka kupigwa marufuku kwa vazi la Kiislamu linalofunika sehemu au uso mzima la Burqa, kukomesha mfumo wa uraia wa nchi mbili, kuweka sheria kali zinazowataka wageni kujumuika katika jamii na kujifunza Kijerumani na vile vile kuweka kiwango cha mwisho cha waomba hifadhi wanaoweza kukubaliwa kuwa laki mbili kwa mwaka.

Chama hicho ambacho mara kwa mara kumeshambulia msimamo laini wa Merkel kuhusu wakimbizi, ambao ulipekelea kupokelewa kwa wakimbizi milioni moja katika taifa hilo kubw azaidi kiuchumi katika Umoja wa Ulaya mwaka uliyopita -- kinapanga kuwasilisha waraka huo katika mkutano unaofanyika siku ya Ijumaa.

Mwenyekiti wa CSU Horst Seehofer amekuwa mkosoaji mkubwa wa seray a Merkel ya wakimbizi, na ametishia kugombea kivyake katika uchaguzi mkuu mwaka 2017 ikiwa Merkel hatobadili muelekeo kuhusu wahamiaji.
Mwenyekiti wa CSU Horst Seehofer amekuwa mkosoaji mkubwa wa seray a Merkel ya wakimbizi, na ametishia kugombea kivyake katika uchaguzi mkuu mwaka 2017 ikiwa Merkel hatobadili muelekeo kuhusu wahamiaji.Picha: picture-alliance/dpa/R. Hirschberger

Hatutaki Waislamu!

Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya chama cha mrengo mkali wa kulia kinachopinga uhamiaji na Uislamu cha Alternative für Deutschland - au Chama Mbadala cha Ujerumani - AfD kukishinda chama cha Merkel cha Christian Democratic Union CDU, katika uchaguzi wa jimbo, na ukiwa umesailia karibu mwaka mmoja kabla ya Ujerumani kufanya uchaguzi mkuu.

Merkel, ambaye umaarufu wake wa muda mrefu umeshuka kufuatia mgogoro wa wakimbizi, siku ya Jumatano alivionya vyama vya siasa dhidi ya kujishusha hadhi kwa kuchukuwa msimamo wa chama cha AfD wa kueneza chuki dhidi ya Uislamu.

Lakini washirika wake wa CSU, chenye makao yake katika jimbo la kusini lenye wahafidhina wengi wa kikatoliki la Bavaria, wameendelea na ukosoaji wao katika waraka huo wa kurasa tano.

"Tunasema wazi kabisaa kwamba wahamiaji wanaotufaa ni wale wenye utamaduni sawa na wa kwetu wa Kikristo na maadili ya Kimagharibi. Tunapata shida kuona idadi kubwa ya watu wa imani na maadili tofauti wakija Ulaya na Ujerumani, na tunajua hisia za watu kuhusiana na suala hilo," alisema katibu mkuu wa CSU Andreas Scheuer, na kuongeza kuwa "laazima Ujerumani ibakie kuwa Ujerumani."

Katibu mkuu wa chama cha CSU Andreas Scheuer ameweka wazi kuwa hawataki wahamiaji Waislamu.
Katibu mkuu wa chama cha CSU Andreas Scheuer ameweka wazi kuwa hawataki wahamiaji Waislamu.Picha: picture-alliance/ZB/K. Schindler

Mbunge CDU aishambulia CSU

Mbunge mwandamizi kutoka chama cha CDU Michael Fuchs amekosoa msimamo huo wa chama cha CSU akisema katika mahojiano ya televisheni, kuwa kila mtu ana haki ya kuja Ujerumani wakiwa wakimbizi wa kweli na iwapo wanatokea katika maeneo hatari, bila kujali iwapo mtu anatokea Aleppo nchini Syria, awe wa madhehebu ya Yazidi, Muislamu au Mkristo.

Wakati huo uhalifu dhidi ya wageni -- yakiwemo mashambulizi, matamshi ya chuki mtandaoni na mashambulizi ya moto dhidi ya makaazi ya wakimbizi umeripotiwa kuongezeka nchini Ujerumani. Mwenyekiti wa baraza kuu la Waislamu la Ujerumani Aiman Mazyek, alisema idadi ya mashambulizi ya kimwili na kimaneno dhidi ya Waislamu imeongezeka katika namna isiyo kifani.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,dpae

Mhariri: Saumu Yusuf