1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Washirika wa Saddam wafikishwa mahakamani leo

Josephat Charo21 Agosti 2007

Kesi dhidi ya wanachama 15 wa utawala wa kiongozi wa zamani wa Irak, Saddam Hussein, imeanza kusilikilizwa hii leo kwenye mahakama inayoungwa mkono na Marekani mjini Baghdad.

https://p.dw.com/p/CB1t
Ali Hassan al Majeed ´Chemical Ali´
Ali Hassan al Majeed ´Chemical Ali´Picha: AP

Makamanda wa zamani wa jeshi la Saddam Husein wamefikishwa mahakamani leo mjini Baghdad kwa kuhusika na ukandamizaji wa mapinduzi ya Washia kusini mwa Irak mwishoni mwa vita vya Ghuba vya mwaka wa 1991. Maelfu ya Wairaki waliuwawa kwenye harakati hiyo iliyofanywa na vikosi vya jeshi la Saddam.

Wengine walioshtakiwa pamoja na maafisa wa jeshi la Irak ni waziri wa zamani wa ulinzi na mwandishi wa Saddam. Mshtakiwa wa ngazi ya juu katika kesi hiyo dhidi ya maafisa 15 wa utawala wa zamani wa Irak ni binamu yake Saddam anayeogopewa sana, Ali Hassan al Majeed, anayejulikana kama Chemical Ali. Washukiwa wote wanakabiliwa na mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu kwa kuhusika na mashambulio dhidi ya umma wa Irak.

Watatu miongoni mwa washtakiwa walihukumiwa kifo katika kesi ya awali ya Anfal kuhusiana na kampeni ya jeshi la Irak dhidi ya Wakurdi wa kaskazini mwa Irak mnamo mwaka wa 1988 ambapo maelfu ya Wakurdi pia waliuwawa. Washukiwa watano wa kesi hiyo ya Anfal wamekata rufaa wakitaka kesi yao isikilizwe upya. Iwapo Majeed na washukiwa wengine wawili waliouhukumiwa kifo watashindwa katika kesi hiyo ya mauaji ya Anfal, huenda wakanyongwa kabla kesi inayowakabili hivi sasa kumalizika.

Mahakama ya mjini Baghdad itawasikiliza mashahidi takriban 90 na kanda za sauti na ripoti zilizotolewa baada ya mauaji hayo ya Washia. Maafisa wa Marekani katika mahakama ya mjini Baghdad wamesema kuna ushahidi kidogo uliosalia wa amri zilizotolewa kwa kuwa Saddam Hussein aliamuru kumbukumbu ziharibiwe.

Licha ya kesi dhidi ya wafuasi wa Saddam Hussein kuanza kusikilizwa leo, Washia wengi nchini Irak bado wanailaumu vikali Marekani kwa kuwasaliti. Kesi hiyo huenda ifufue mjadala juu ya uamuzi wa rais wa zamani wa Marekani, George Bush, wa kutoivamia Irak baada ya kuyalazimisha majeshi ya Irak yaondoke Kuwait wakati wa vita vya Ghuba vya mwaka 1991.

Kwa kuwa Saddam Hussein hakukabiliwa na kitisho cha kuvamiwa, aliweza kutumia vikosi vya jeshi lake kuyakandamiza kwa haraka mapinduzi ya waislamu wa madhehebu ya Shia kusini mwa Irak na mapinduzi ya Wakurdi kaskazini mwa nchi hiyo, yaliyozuka siku chache baada ya vita vya Ghuba kumalizika mnamo tarehe 28 mwezi Februari mwaka wa 1991.

Terehe 16 mwezi Februari mwaka wa 1991, siku chache kabla mapinduzi kuanza mwanzoni mwa mwezi Machi, rais mustaafu wa Marekani, George Bush, alilitolea mwito jeshi la Irak na Wairak wachukue hatua za kumshinikiza Saddam aondoke madarakani.

´Ni njama ya Wamarekani. Jana waliviruhusu vikosi vya Saddam kushambulia katikati na kusini mwa Irak na leo wanawashitaki kwa mauaji ya halaiki, ´amesema kwa hasira Dhiya Hussein, mkaazi wa mji mtakatifu wa Najaf nchini Irak, mwenye umri wa miaka 44.

Rais mustaafu George Bush amekuwa akisema wakati alipokuwa na matumaini kwamba mapinduzi dhidi ya Saddam yangemuondoa kiongozi huyo madarakani, hakutaka kuona taifa la Irak likisambaratika. Aidha George Bush anasema alihofia kuvunjika kwa jeshi la muungano aliloliunda, ambalo lilijumulisha pia nchi za kiarabu.

´Hutaka tu nicheke ninaposikia wabunge wa Marekani wakizungumzia kueneza demokrasia katika eneo la Mashariki ya Kati,´ amesema Mohammed al Jawahiry, daktari mwenye umri wa miaka 32 katika mji wa Basra kusini mwa Irak. Daktari huyo ameuliza kwa nini Wamarekani walimruhusu Saddam kuwaua wanawake na watoto wakati Wairaki walipofanya mapinduzi kupinga utawala wake wa kiimla.

Saddam Hussein aliangushwa madarakani wakati wa uvamizi wa Irak mnamo mwezi Machi mwaka 2003 na rais wa sasa wa Marekani George W Bush akachukua hatua moja mbele kuliko babake George Bush kwa kusema Irak ilikuwa na silaha za maangamizo ambazo mpaka leo hazijapatikana.

Sambamba na hayo, polisi mjini Basra leo wamegundua kaburi la halaiki lililokuwa na mabaki ya maiti za vijana 15 waliouwawa wakati wa mapinduzi ya mwaka wa 1991. Msemaji wa polisi mjini humo, kanali Karim Rheima, amesema maiti hizo zina majeraha ya risasi vicwani na walioshuhudia wanasema vijana hao waliuwawa na vikosi vya mauaji vya Saddam.