1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

'Washirika' wa vita vya Libya wakutana Doha

13 Aprili 2011

Baraza la Kitaifa, chombo cha kisiasa cha la waasi wa Libya, linakutana na jumuiya kimataifa mjini Doha kusisitiza ulazima wa Muammar Gaddafi kuondoka kwa maslahi ya amani na pia kutafuta kutambuliwa rasmi.

https://p.dw.com/p/10sMJ
Kiongozi wa Baraza la Mpito, Mustafa Abdul Jalil
Kiongozi wa Baraza la Mpito, Mustafa Abdul JalilPicha: picture alliance/dpa

Msemaji wa Baraza hilo la mpito, Mahmud Shammam, amesisitiza kwamba Baraza lake halitakubali jambo lingine lolote ila kuondoka madarakani kwa Kanali Gaddafi na wanawe.

Shammam ameeleza kuwa Baraza lake linataka kutambuliwa na jumuiya ya kimataifa kuwa ndiyo serikali halali ya watu wa Libya.

Amesema kwanza wanataka jumuiya ya kimataifa itambue hali halisi kwamba Baraza hilo lipo, na pili, Baraza hilo litambuliwe kuwa mwakilishi halali duniani.

Hayo yatakuwa mapendekezo makubwa ya Baraza hilo kwenye mkutano wa mjini Doha, Qatar, kwa jopo la wajumbe wa kimataifa wanaowasiliana na na kufanya kazi waasi wa Libya.

Mpaka sasa Baraza hilo linaloendesha shughuli zake kutokea mji wa Benghazi linatambuliwa na Ufaransa, Italia na Qatari tu.

Ikiwa Baraza hilo litatambuliwa na jumuiya kimataifa, litaweza kupatiwa mambilioni ya fedha zilizozuiwa nchini Marekani na Uingereza, aidha litakuwa na haki ya kupatiwa mikopo katika msingi wa viwango vya kiserikali .

Mwakilishi wa Baraza la Kitaifa kwa Mambo ya Nje, Ali al-Essawi
Mwakilishi wa Baraza la Kitaifa kwa Mambo ya Nje, Ali al-EssawiPicha: dapd

Jopo la kimataifa linalowasiliana na waasi wa Libya lililoundwa mjini London wiki mbili zilizopita, kwa mara ya kwanza litatafakari njia za kuleta amani nchini Libya.

Lakini msemaji wa serikali ya Libya ameudhihaki mkutano wa Doha, akisema kuwa mkutano huo unafanyika Qatar nchi ambayo ni kama kampuni ya mafuta na sio taifa la dhati. Na ameitaka dunia isidanganyike na alichokiita kuwa ni uongo wa Qatar.

Mkutano wa Doha pia utajadili mchango wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO katika harakati za kupambana na Gaddafi hasa kutokana na lawama zilizotolewa na Ufaransa na Uingereza kwamba Jumuiya hiyo haifanyi ya kutosha kuwalinda raia.

Madai haya yamekanushwa na Kamanda wa NATO, Jenerali Mark Van Uhm, ambaye anasema kuwa sasa majeshi ya Gaddafi hayana uwezo wa kufanya yapendavyo, licha ya kukiri kwamba bado kazi ingalipo.

"Hawawezi kupigana jinsi wapendavyo na wala hawawezi kuzitumia silaha wazipendazo. Hata hivyo, hakuna cha kuashiria kwamba Gaddafi anadhamiria kuacha mapambano." Amesema Jenerali Van Uhm.

Mkutano huu wa mjini Doha unahudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, ambaye nchi yake inapinga hatua za kijeshi dhidi ya Libya, ingawa iko tayari kushiriki kwenye huduma za kibinaadamu kama vile matibabu na uokozi.

Wengine watakaohudhuria ni wawakilishi kutoka Umoja wa Ulaya, Umoja wa Mataifa, Marekani na wale wa kutoka Umoja wa Nchi za Kiarabu.

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya, Mousa Kuossa, pia atadhuhuria mkutano wa Doha.

Mwandishi: Abdu Mtullya/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman