1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Washukiwa wa machafuko ya London kufikishwa mahakamani leo

14 Agosti 2011

Ni washukiwa wa kwanza kushtakiwa kwa vifo vilivyotokea wakati wa machafuko ya jijini London. Watu jumla ya watano walikufa kwenye machafuko yaliyoanza Jumamosi iliyopita.

https://p.dw.com/p/12GD2
Hali ilivyokuwa mashariki mwa LondonPicha: dapd

Mwanamume mmoja pamoja na kijana wanatarajiwa kufikishwa katika mahakama moja ya Birminghman leo kuhusiana na mauaji ya wanaume watatu waliogongwa na motokaa wakati walipokuwa wakikilinda kitongoji chao dhidi ya waporaji. Ni washukiwa wa kwanza kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria kwa vifo vilivyotokea wakati wa maandamano mabaya kabisa kuwahi kushuhudiwa nchini Uingereza katika kipindi cha miongo kadhaa.

Hapo awali polisi walisema wamepata motokaa mbili katika uchunguzi wao na kupata vizibiti 400 na taarifa zaidi ya 70 za mashahidi.

London Krawalle
Polisi wakipiga doria LondonPicha: dapd

Haroon Jahan, mwenye umri wa miaka 20, Shazad Ali mwenye umri wa miaka 30, na kakake Abdul Musavir, mwenye umri wa miaka 31, waliuwawa Jumatano iliyopita kwenye lango la kituo cha mafuta kwenye kitongoji cha Winson Green huko Birmingham. Babake Jahan, Tariq, amepongezwa kwa mwito wake wa kuwataka watu wasilipize kisasi kifo cha mwanawe. Polisi wamekiri mwito wake huo umesaidia kutuliza hisia za watu, huku ukukiwa na wasiwasi kuhusiana na uhusiano kati ya jamii za Burmingham.

Mbali na vifo vitatu vilivyotokea huko Birmingham, watu wengine wawili walikufa katika wimbi hilo la machafuko yaliyoanza mjini London Jumamosi wiki iliyopita na kuenea katika miji mingine mikubwa ya Uingereza.

Mwansishi: Josephat Charo

Mhariri:Prema Martin