1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Washukiwa wawili wa ugaidi wakamatwa uwanja wa ndege wa Cologne

26 Septemba 2008

-

https://p.dw.com/p/FPT7
Picha: picture-alliance/ dpa

Watu wawili wanaoshukiwa kuwa ni magaidi wametiwa nguvuni hivi punde katika uwanja wa ndege wa Cologne hapa nchini Ujerumani.

Watu hao walikamatwa baada ya polisi wa ujerumani kuivamia ndege ya shirika la ndege la KLM kabla haijaruka.

Polisi ya Ujerumani imesema kwamba makamando wamewakamata washukiwa hao wawili wa ugaidi katika uwanja wa ndege wa Kolon kabla ya ndege waliokuwa wamepanda kuondoka kuelekea Armsterdam.

Polisi wa jimbo la North Rhine Westphalia imesema kuwa washukiwa hao ni raia mmoja wa Somalia mwenye umri wa miaka 23 na mwenzake mjerumani mzaliwa wa Somalia aliye na umri wa miaka 24.

Walikamatwa wakiwa ndani ya ndege ya KLM kabla ya ndege hiyo kuruka kuelekea Armsterdam.

Msemaji wa shirika hilo la ndege la KLM amezungumza na shirika moja la habari la uholanzi na kusema kuwa polisi walipanda ndege hiyo wakati ambapo ilikuwa tayari ndege hiyo inajiandaa kuanza safari yake na kuwakamata washukiwa hao wawili.

Aidha amesema kwamba tukio hilo lilimlazimu kila abiria aliyekuweko ndani ya ndege hiyo kukimbia na vile vile kusababisha msongamano ´wa foleni ya kusubiri mizigo ambapo kila mmoja alitaka kuchukua mzigo wake.

Gazeti maarufu la humu nchini la Bild limenukuu taarifa kutoka duru za polisi zikisema kwamba wawili hao walikuwa wakichunguzwa mienendo yao kwa muda wa miezi kadhaa sasa na kumeweza kukutikana kijibarua ndani ya nyumba yao waliyokuwa wanaishi kilichokuwa kimeandikwa juu ya wawili hao kutaka kujitoa muhanga.

Ndani ya kijibarua hicho washukiwa hao wameeleza nia yao ya kutaka kufa katika vita vitakatifu.

Kijibarua hicho kinaelezwa kuwa huenda kilikuwa ni ujumbe wa mwisho wa washukiwa hao kabla ya kwenda kutekeleza mashambulio ya kigaidi.

Wakati huo huo polisi wamewakamata rasmi vijana watatu waliowavamia polisi wawili mjini Cologne mnamo wiki hii.

hapo mapema gazeti la Koelner Rundschau linalotoka kila siku liliripoti kwamba vijana hao wenye umri wa miaka 15,16 na 17 wakiwa na asili ya wahamiaji walirudia matamshi ya Vita vitakatifu"Jihadi" wakati walipokua wakihojiwa.

Hata hivyo msemaji wa ofisi ya mwendesha mashitaka mjini Cologne Tino seesko hakuthibitisha ripoti za vyombo vya habari vilivyodai shambulio hilo lilitokana na hisia za watu wenye msimamo mkali.