1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasichan wa Ujerumani mabingwa wa ulaya

11 Septemba 2009

Semenya si mwanamke si mwanamume ?

https://p.dw.com/p/Jd5M
Birgit Prinz akisherehekea ushindi.Picha: AP

-Kombe la klabu bingwa barani Afrika larudi uwanjani mwishoni mwa wiki hii huku TP Mazembe ikitembelea Heartland huko Nigeria.

-Mtogo Emmanuel Adebayor aliehamia Manchester city anapambana leo na klabu yake ya zamani Arsenal London katika Premier-League.

Miroslav Klose alietia mabao 2 kati ya wiki katika ushindi wa mabao 4-0 wa Ujerumani dhidi ya Azerbaijan atazamia kurejeshwa leo uwanjani munich ikicheza na Borussia Dortmund katika Bundesliga.

-Timu ya taifa ya wasichana ya Ujerumani kwa mara nyengine ni mabingwa wa dimba wa Ulaya.

Na waziri wa michezo wa Afrika kusini akasirishwa na taarifa za vyombo vya habari vya Australia kuwa bingwa wao wa mita 800 Caster Semenya ni" upande mwanamke na upande mwanamume".Je, atavuliwa taji la dunia ?

BUNDESLIGA:

Mabingwa Wolfsburg wanapambana leo na Leverkusen iliopo nyuma ya Hamburg na nafasi ya pili ya ngazi ya Ligi.Bundesliga-Ligi ya Ujerumani inarudi uwanjani jioni hii huku viongozi wa Ligi-Hamburg wakicheza na Stuttgart,mabingwa mara kadhaa Bayern Munich wana miadi na Borussia Dortmund.Stadi wa Munich,Miroslav Klose anatumai kugonga tena leo vichwa vya habari kufuatia mabao yake 2 juzi pale Ujerumani ilipocheza na Azerbaijan na kushinda kwa mabao 4:0.Schalke itakuwa kesho mjini Cologne inayoburura mkia wa Ligi.Bremen iliopo nafasi ya 3 ya orodha ya Ligi inacheza nyumbani na jirani yake wa kaskazini Hannover.

TIMU YA TAIFA YA WANAWAKE MABINGWA WA ULAYA:

Timu ya wasichana ya Ujerumani imetamba tena katika dimba la ulaya .Katika finali na Uingereza mjini Helsinki,Finnland juzi , wasichana wa Ujerumani waliwakandika wale wa Uingereza mabao 6:2 na kutoroka tena na Kombe.

Hii ni mara ya 5 kwa timu ya Taifa ya wanawake ya Ujerumani , mabingwa mara 2 wa dunia, kuvaa taji la ulaya tena mfululizo.Mabao 2 ya Brigit Prinz na 2 ya Inka Grings,moja la Melanie Behrunger na Kim kulig, yalitosha kulirudisha Kombe hilo nyumbani Frankfurt.Grings kutoka duisburg kwa mabao yake 6 kama katika kombe la ulaya 2005 huko Uingereza, ameibuka mtiaji mabao mengi katika Kombe hili la ulaya.

Ushindi wa wasichana wa Ujerumani ulipongezwa mno na Rais Horst Kohler wa ujerumani aliekuwa uwanjani kuangalia finali hiyo pamoja na rais wa Shirikisho la dimba la Ujerumani Theo Zwanziger.

Ushindi huu ni muhimu sana kwavile,Ujerumani ndio inayoandaa Kombe la dunia la wanawake 2011. Walipowasili nyumbani alaasiri ya jana ,timu nzima ilipokewa kwa shangwe na shamra-shamra katika ukumbi wa mji wa Frankfurt,tayari kwa sherehe ya ushindi. Kila mchezaji wa timu hiyo ametunukiwa kitita cha Euro 10.000.

MKASA WA BINGWA WA MITA 800 CASTER SEMENYA:

Waziri wa michezo wa Afrika kusini,Makhenkesi Stofile, alisema jana kuwa amestushwa na kukasirishwa mno na ripoti za vyombo vya habari vya Australia kuwa uchunguzi juu ya Caster Semenya umeonesha yeye ni "hermaphorodite"-yenye maana sehemu ni "mwanamume na sehemu ni mwanamke". Akasema jaribio lolote la kumzuwia kushindana katika mashindano ya wanawake kutazusha vita vya tatu vya dunia.

Waziri huyo wa Afrika Kusini akalituhumu shirikisho la riadha ulimwenguni IAAF kukiuka haki za binadamu kwa kuhoji iwapo Semenya ni mwanamke au mwanamume na kwamba serikali ya Afrika kusini imekipeleka kisa hiki kwa mawakili wake.

Akihutubia mkutano na waandishi habari jana mjini Pretoria, waziri Stofile alilituhumu Shirikisho la riadha ulimwenguni (IAAF) kutumia vyombo vya habari kufichua matokeo ya uchunguzi aliofanyiwa Semenya wakati huo huo likijadi haijui chochote.

Akasema ni wazi kwao kuwa haki za binadamu za Semenya zinakiukwa na si yeye Semenya wala wazee wake wanostahiki kutendewa hayo,kwani hakuna ovu walilofanya.Shirikisho la riadha ulimwenguni IAAF liliamuru Semenya afanyiwe uchunguzi iwapo kweli ni mwanamke mapema msimu huu wa riadha.Taarifa juu yake zilivuja masaa kabla ya finali ya mbio za mita 800 mjini Berlin,August 19.

Shirikisho la riadha ulimwenguni (IAAF) liliarifu jana kwamba limeshapokea matokeo ya uchunguzi aliofanyiwa Semenya ,lakini halitasema chochote juu yake hadi uamuzi wa mwisho umepitishwa na Baraza la shirikisho hilo linalokutana hapo Novemba 20 na 21 mjini Monte Carlo,makao yake makuu.

Caster Semenya alianza kugonga vichwa vya habari katika medani ya riadha mwaka huu 2009.Muda wake wa kasi katika mbio za mita 800 na umbo lake la kiume, ulisababisha Shirikisho la riadha dunia-IAAF kuamrisha achunguzwe ni mwanamke au mwanamume. Je, sasa taji lake la mbio za mita 800 atavuliwa ? Atashindana upande gani siku zijazo ule wa wanawake au wanaume ? Au hatashindana kabisa ?Novemba tutajua zaidi.

Mwandishi:Ramadhan Ali/ AFPE/DPA

Mhariri:M.Abdul-Rahman